Spika wa Bunge Kenya aamuru uchunguzi wa mauaji ya mbunge, Charles Ong’ondo
(last modified Thu, 01 May 2025 07:00:46 GMT )
May 01, 2025 07:00 UTC
  • Moses Wetang’ula
    Moses Wetang’ula

Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya, Moses Wetang’ula amemwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kuchunguza mara moja mauaji ya mbunge wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were na kuwasilisha matokeo ya uchunguzi huo bungeni bila kuchelewa.

Wetang’ula amemtaja Were kuwa alikuwa mnyenyekevu, mwenye heshima na asiye na mabishano, na kusema asili ya mauaji hayo inaashiria mmomonyoko wa maadili unaotia wasiwasi nchini.

Pia ametaka ulinzi uimarishwe kwa viongozi na Wakenya wote.

Charles Ong’ondo Were, ambaye alikuwa mbunge wa chama cha ODM aliuawa hapo jana kwa kupigwa risasi jijini Nairobi na watu waliokuwa wakilifuata gari lake.

Charles Ong’ondo Were

Mbunge huyo aliyewakilisha eneo Bunge la Kasipul, alipigwa risasi na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki kwenye barabara ya Ngong majira ya saa moja na nusu jioni.

Mauaji yake yametokea karibu miezi mitatu tangu adai kuwa maisha yake yako hatarini kufuataia matukio ya ghasia katika eneo Bunge lake, ambazo alidai zilichochewa na vyanzo kutoka nje.

Watu walioshuhudia walisema, mmoja wa washambuliaji hao alishuka kwenye pikipiki na kumfyatulia risasa mbunge huyo na kumjeruhi vibaya, kabla ya kukimbizwa hospitalini.