Mpango wa sarafu moja ya Sahel badala ya CFA Franc ya Ufaransa
Niger imeandaa mkutano wa kuendeleza sarafu ya pamoja ya Muungano wa Nchi za Sahel (AES), kwa sababu uhuru wa kweli hauwezekani bila mamlaka ya kifedha.
Abdourahamane Oumarou ambaye ni mwanaharakati wa kutetea umajumui wa Africa amehudhuria kongamano na kusema sarafu ya CFA Franc inayotumiwa na nchi za Magharibi na Kati mwa Afrika ndiyo sarafu pekee ya kikoloni inayotumika hadi leo — jambo ambalo amesema haliwezi kuwa la kawaida.
Wakati mapambano ya kideolojia ya kujiondoa katika minyororo ya ukoloni hapo awali yaliongozwa na wanaharakati mitaani, mjadala huo sasa umehamia kwenye mazungumzo ya kidiplomasia katika kumbi za mikutano, amesema mwanaharakati huyo kando ya mkutano wa kupinga sarafu ya CFA Franc.
Mkutano huo, uliofanyika mjini Niamey, Niger, ni muhimu ili kuwapa viongozi wa Afrika “mwelekeo wa kweli, ramani ya barabara itakayowaongoza” kwenye njia ya kuelekea uhuru kamili, alisisitiza.
“Siku itafika bila shaka ambapo viongozi wetu watalazimika kutumbua jipu hili na hatimaye kuondokana na minyororo ya ubeberu, minyororo ya sarafu hii ya kikoloni,” ameongeza Oumarou.
Muungano wa Nchi za Sahel (AES) ni shirikisho lililoundwa kati ya Mali, Niger, na Burkina Faso ambalo liliundwa baada ya mkataba wa ulinzi wa pamoja uliosainiwa tarehe 16 Septemba 2023, kufuatia mzozo wa kisiasa wa Niger mwaka huo ambayo ilifanya Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kutishia kuingilia kijeshi kurejesha utawala wa kiraia baada ya mapinduzi nchini Niger.
Sarafu hiyo ambayo ilitambulishwa na Ufaransa 1945, inatumika kwa muda mrefu katika nchi nyingi za Afrika na sasa kuna harakati ya kuta itupiliwe mbali.