Makosa 6 makubwa ya kimkakati ya Marekani kuhusu Iran
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, Marekani ikiwa kiongozi wa nchi za Magharibi, muda wote imekuwa ikilifanyia uadui taifa la Iran katika kipindi cha miaka 46 sasa ikiwa ni pamoja na kuliwekea vikwazo vikubwa kupindukia. Hata hivyo Washington imeshindwa kufikia malengo yake dhidi ya Iran.
Yafuatayo ni baadhi ya makosa makubwa ya kiistratijia yaliyofanywa na Marekani katika uadui wake dhidi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
1- Jaribio la kuipindua Jamhuri ya Kisilamu na kurejesha utawala kibaraka nchini Iiran:
Kosa la kwanza la kiistratijia la Marekani ni kwamba inadhani kuwa inaweza kwa mara nyingine kuigeuza Iran kuwa kibaraka wa Washington katika ukanda huu ili kuendelea kulinda maslahi yake haramu na kupunguza gharama zake za usalama katika eneo hili. Lakini dhana hii chapwa inaonesha kwamba Wamarekani hawana ufahamu wa kina wa historia ya taifa la Iran, ambalo ni moja ya vyanzo vinavyounda utamaduni wa kimkakati wa Iran. Katika historia yao yote, Wairani hawajawahi kuwa kibaraka wa mtu yeyote, isipokuwa kwa muda mfupi tu, na daima wamekuwa tayari kuvumilia kila aina ya mashaka na matatizo, lakini si kupoteza uhuru na heshima yao. Katika kipindi kifupi cha utawala kibaraka wa Pahlavi II, ulioanza baada ya mapinduzi ya Agosti 19, 1953, watawala hao wa Iran walikubali kuwa vibaraka wa Magharibi, lakini hawakudumu muda mrefu yaani ukibaraka wao uliharakisha kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Iran na kuporomoka utawala wa Pahlavi. Kwa hiyo, jaribio lolote la kurejesha ukibaraka mchini Iran litashindwa tu.
2- Kupuuza nafasi ya dhati ya Iran katika eneo hili:
Kosa la pili la kiistratijia la Marekani ni kupuuza nafasi ya asili na ya dhati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye ukanda huu. Maana ya nafasi ya asili na ya kimaumbile ya Iran katika eneo la Asia Magharibi haiishii tu katika nyoyo za watu wa jamii ya Kishia za eneo hili, bali nafasi na hadhi ya Iran inatokana na fikra zake pana na msimamo usiofungwa na mipaka ya dini na madhehebu. Ni nafasi ya historia na ustaarabu, bali kwa hakika, ni hadhi na heshima yake kiutamaduni. Nafasi ya kweli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili inatokana na kwamba Jamhuri ya Kiislamu haiwabebeshi watu wa eneo hili gharama za kiuchumi na wala haifikirii masuala yake binafsi bali inachojali ni maslahi ya watu wenyewe wa maeneo hayo na haiingilii maamuzi yao.
3- Kupuuza mafasi kubwa ya Iran katika kuimerisha usalama:
Kosa jengine la kiistratijia la Marekani katika uadui wake dhidi ya Iran ni kwamba Washington inafanya njama za kukhafifisha nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuimarisha usalama na amani hususan katika vita dhidi ya ugaidi na magenge yenye misimamo mikali. Kwa maneno mengine ni kwamba, uzoefu wa miaka michache iliyopita katika eneo hilo umeonesha kwamba hakuna serikali katika eneo hili yenye utashi wa kisiasa, uwezo wa kimkakati, au uwezo wa kijiografia unaohitajika na wa kutosha wa kuweza kukabiliana vilivyo na magenge ya kigaidi na ya ukufurishaji ghairi ya Iran. Lau kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isingekuwa nguvu kubwa ya eneo hili, magenge ya ukufurishaji na ya kigaidi yangepata nguvu zaidi na usalama wa eneo hili zima ungepotea.
4- Vikwazo na mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran:
Kosa jengine ambalo Marekani imelifanya katika uadui wake dhidi ya Iran ni kuiwekea Tehran vikwazo vikubwa hasa baada ya Marekani kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2018. Wakati huo ilijaribu kuilazimisha Iran kubadilisha misimamo yake kupitia "mashinikizo ya juu zaidi." Lakini njama hizo za Marekani si tu zilishindwa tangu zamani, lakini pia ziliimarisha Muqawama ndani ya Iran, zilipelekea kufanyika jitiihada kubwa zaidi za kujitosheleza humu nchini kiasi kwamba katika baadhi ya masuala, Iran imeweza kupiga hatua kubwa kuliko nchi zote duniani. Vikwazo hivyo vya juu zaidi vimezidi tu kutoaminiana kati ya Iran na Marekani hasa kwa sababu vina taathira hasi kwa maisha ya watu wa kawaida na haviwezi kabisa kuilazimisha Jamhuri ya Kiisilamu kubadilisha misimamo yake ya haki.
5- Kujaribu kuifanya Iran itengwe kieneo na kimataifa:
Marekani imekuwa ikifanya njama muda wote za kujaribu kuifanya Iran itengwe katika eneo hilo lakini sera zake mara nyingi zimekuwa zikipingana. Lakini pamoja na mashinikizo hayo, Iran imedumisha na hata kuimarisha uhusiano wake na nchi kama vile Russia, China na baadhi ya majirani wa eneo hili. Pia, ushawishi wa Iran nchini Iraq, Lebanon kupitia Muqawama wa wananchi wa nchi hiyo, Yemen sambamba na Muqawama wa Wapalestina umefanya njama za Marekani za kujaribu kupunguza nafasi na ushawishi wa Iran katika eneo la Asia ya Magharibi kuwa duni na kusambaratika.
6- Kukosa Marekani kuheshimu ahadi zake, kudharau diplomasia endelevu na kubadili msimamo mara kwa mara
Sera ya kigeni ya Marekani kuhusu Iran mara nyingi imekuwa ikiyumba. Kwa mfano, katika zama za Obama, Marekani ilijiunga na JCPOA, lakini ilijiondoa katika JCPOA wakati wa Trump. Katika zama za Biden, ingawa kulikuwa na nia ya kurejea JCPOA lakini Marekani haikurejea kwenye ahadi zake katika makubaliano hayo. Hivi sasa katika muhula wake wa pili kama rais, Trump kwa mara nyingine tena amepitisha sera ya mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran ingawa wakati huo huo imeanza kufanya mazungumzo na Iran.
Kiujumla ni kwamba, makosa makubwa ya Marekani dhidi ya Iran yanaonyesha kuwa kukabiliana na Iran bila ya kuzingatia matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama ya taifa hili hayawezi kuleta matokeo inayoyataka Washington. Wachambuzi wengi wanaamini kuwa Washington inahitaji mkakati wa kweli zaidi na endelevu kuhusu Tehran. Makosa ya kiistratijia ya Marekani dhidi ya Iran yanaonesha pia kwamba, mahesabu mabaya ya wachukua maamuzi huko Marekani yamekuwa muda wote yakiifelisha Washington na viongozi wake.