Nchi mbalimbali zalaani mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela
-
Hujuma ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela
Nchi mbalimbali duniani zimeendelea kulaani vikali mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela. Nchi hizo zimeeleza wasiwasi wao kuhusu uhalali, maadili na taathira hatari za uvamizi wa Marekani huko Venezuela.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana Jumamosi ilisisitiza katika taarifa yake kwamba: inalaani vikali mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela na ukiukaji mkubwa wa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya nchi hiyo.
Russia kwa upande wake imepinga na kulaani mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela na kuyataja kuwa haramu na kinyume cha sheria. Konstantin Kosachev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Shirikisho la Russia ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa Telegram akisema kwamba: Venezuela haikuwa tishio kwa Marekani, na kwamba sheria za kimataifa ndizo zinazopaswa kufuatwa, na si sheria za kujibunia”.
Rais Miguel Diaz- Canel wa Cuba ameyataja mashambulizi ya Marekani dhidi ya Caracas kuwa kitendo cha jinai na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.
Colombia pia imesema inapinga hatua za upande mmoja za kijeshi na imesisitiza kuwa nchi hiyo inaendelea kuheshimu mkataba wa Umoja wa Mataifa hususan kipengee kinachotaja kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala nchi na kuzuia matumizi ya nguvu.
Serikali ya Uhispania kwa upande wake imesema kuwa iko tayari kusaidia jitihada za kupunguza mivutano na imetaka kuheshimiwa sheria za kimataifa. Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uhispania imesisitiza kuwa ipo haja ya kuzuia machafuko zaidi na kwamba ipo tayari kuwa mpatanishi ili kufanikisha mazungumzo na ufumbuzi wa amani.
Naye Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa Italia amesema amekuwa akifuatilai kwa karibu hali ya mambo ya Venezuela akijikita hasa katika kukusanya taarifa kuhusu raia wa Italia wanaoishi Venezuela. Amesema, kwa wastani Wataliano 160,000 wanaoishi Venezuela aghalabu yao wana uraia wa nchi mbili.
Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva amesema: Kushambulia ardhi ya Venezuela na kumkamata rais wake kunavuka mstari usiokubalika na kwamba kitendo hicho ni dharau kubwa kwa mamlakka ya kujitawala Venezuela na mfano hatari sana kwa jamii ya kimataifa.
da Silva amesema: Kushambulia nchi zinazojitawala ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na hatua ya kwanza kuelekea ulimwengu wa vurugu, machafuko na ukosefu wa utulivu.
Ameongeza kuwa, mashambulizi hayo yanakumbusha nyakati mbaya zaidi za uingiliaji kati wa kisiasa wa Marekani katika nchi za Amerika Kusini na Karibea.