"Uvamizi wa Israel Syria hautayaacha salama mataifa ya Kiarabu, Kiislamu"
Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imesema kuwa, uvamizi wa Israel dhidi ya Syria ni hujuma za dhidi ya mataifa yote ya Kiarabu na Kiislamu hususan Palestina, Lebanon na Syria, na kwamba maeneo mengine ya Kiarabu hayatakuwa salama kutokana na chokochoko hizo na matokeo yake.
Harakati hiyo ya Wapalestina imesema inautazama uchokozi huo wa Wazayuni dhidi ya Syria kuwa kielelezo cha mipango ya kujitanua ya utawala huo pandikizi katika eneo la Asia Magharibi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina Sama, Harakati ya Jihadul Islami katika taarifa yake imelaani vikali mashambulizi na hujuma zinazoendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel katika ardhi ya Syria.
Imesema hujuma hizo ni ushahidi wa wazi wa mipango ya kivamizi na ya kujitanua ya utawala unaoukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina, dhidi ya mataifa ya Kiarabu na Kiislamu ndani ya fremu ya kuligawanya eneo hili vipande vipande.
"Uchokozi wa utawala huu wa kihalifu dhidi ya Syria ni uchokozi wa moja kwa moja, sio tu dhidi ya taifa la Syria lakini pia dhidi ya mataifa yote ya Kiarabu na Kiislamu, haswa Palestina, Lebanon na Syria; na maeneo mengine ya Kiarabu hayatasalimika kutokana na uchokozi huu na matokeo yake," imesema taarifa ya Jihadul Islami.
Aidha Harakati ya Jihadul Islamu ya Palestina imetoa wito wa kuwepo umoja wa makundi yote yakiwemo makundi ya Muqawama ili kukabiliana na hujuma hizo, kukwamisha malengo yao na kulitetea taifa hilo la Kiarabu na Kiislamu (Syria) na adhama yake.