Wanajeshi wawili wa Israel wauawa kwenye mtego katika handaki Gaza
Jeshi katili la Israel limeripoti kwamba wanajeshi wake wawili wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa kutokana na mlipuko katika handaki lililowekwa mitego katika jiji la Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Jeshi vamizi la Israel lilisema Jumapili kwamba Kapteni Noam Ravid (miaka 23) na Sajenti Yaly Seror (miaka 20), kutoka kikosi maalum cha uhandisi wa kivita cha Yahalom, walikuwa wakikagua mlango wa kuingilia kwenye handaki lililopo ndani ya jengo wakati bomu lililkuwa katika mtego lilipolipuka Jumamosi.
Jeshi hilo vamizi la Israel limeongeza kuwa wanajeshi wengine wawili kutoka kikosi hicho walijeruhiwa kwenye mlipuko huo, mmoja wao akiwa katika hali mahututi.
Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, baada harakati ya Hamas ya kupigania ukombozi wa Palestina kufanya operesheni ya kihistoria dhidi ya utawala huo unaoendelea kunyakua ardhi, ikiwa ni jibu kwa ukandamizaji uliokithiri dhidi ya watu wa Palestina.
Licha ya mauaji ya angalau Wapalestina 52,495 — wengi wao wakiwa wanawake na watoto — na kujeruhi zaidi ya 118,366, utawala wa Tel Aviv umeshindwa kufikia malengo yake yaliyotangazwa wazi Gaza. Hatimaye, utawala huo ulikubali masharti ya muda mrefu ya mazungumzo ya Hamas chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalianza Januari 19.
Hata hivyo, miezi miwili baadaye, Israel ilivunja makubaliano hayo kwa upande mmoja na kurejelea mashambulizi yake makali ya anga dhidi ya Gaza.
Zaidi ya wanajeshi 850 wa Israel wameuawa katika mashambulizi hayo dhidi ya Gaza, wakiwemo 414 waliopoteza maisha katika operesheni ya nchi kavu dhidi ya eneo hilo lililowekwa mzingiro.
Katika tukio jingine Jumamosi, jeshi la Israel lilitangaza kwamba linatuma maelfu ya maagizo ya kuwaita askari akiba wa ajili ya maandalizi ya mashambulizi makubwa zaidi Gaza.
Mwito huu wa kuwaita askari akiba unafuatia ripoti kwamba jeshi la utawala huo limewasilisha kwa waziri mkuu Benjamin Netanyahu mpango wake wa mashambulizi ya awamu kwa awamu, ambayo itahitaji idadi kubwa ya askari.
Ripoti hizo zimeibua wasiwasi miongoni mwa familia za mateka wa Israel ambao bado wanashikiliwa Gaza.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, jukwaa la familia za mateka lilionya kwamba kushadidi vita kutaweka mateka hao kwenye hatari ya moja kwa moja.