Baada ya Trump kulegeza msimamo, sasa China yamwekea masharti
China imeiwekea Washington masharti ya mazungumzo baada ya vita vya biashara na ushuru vilivyoanzishwa na Donald Trump kushindwa kuwa na taathira zilizotarajiwa mbali na kusababisha vurugu katika masoko ya fedha ya Marekani, jambo ambalo limemlazimisha Trump alegeze tena misimamo na kudai anataka mazungumzo na Beijing.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, China imetangaza kuwa imepokea maombi ya mazungumzo kutoka kwa Marekani lakini inabidi kwanza ikae na kufikiria maombi hayo hasa hatua ya Trump ya kuziwekea bidhaa za China ushuru wa asilimia 145.
Aidha Beijing imeionya Washington kwamba haiko tayari kulegeza msimamo wake na wala haitokubaliana na masharti yoyote yatakayowekwa na Marekani katika mazungumzo hayo. Msimamo huo wa China umekuja huku mvutano wa biashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani ukiongezeka na kuathiri masoko ya kimataifa.
Maafisa wa China wamesema kuwa, hivi karibuni Marekani imetumia njia mbalimbali kujaribu kuifikia Beijing na ombi la kuanza mazungumzo. China imesema kuwa mlango uko wazi kwa mazungumzo, lakini Marekani lazima ionyeshe nia njema kwa kuondoa kwanza nyongeza ya ushuru iliyoiweka kwa bidhaa za China bila ya sababu yoyote. Wizara ya Biashara ya China imesisitiza kuwa mashinikizo au masharti yoyote kutoka kwa Marekani yatakwamisha tu mazungumzo na hayatokuwa na matokeo mengine ghairi ya mkwamo.
Mvutano ulianza baada ya Marekani kuziwekea bidhaa za China ushuru mkubwa wa asilimia 145. Kwa upande wake, China ilijibu hatua hiyo mwezi Aprili kwa kuziwekea bidhaa za Marekani ushuru wa asilimia 125. Wataalamu wanasema ushuru huo mkubwa unaweza kukwamisha kikamilifu biashara kati ya nchi hizo mbili. Jana Ijumaa serikali ya Marekani iliondoa ushuru kwa baadhi ya bidhaa za China na Hong Kong.
Kwa upande wake, Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Besant amesema ana imani kuwa China inataka kufikiwe makubaliano na anataraji kwamba mazungumzo yataendelea katika hatua kadhaa.