Araghchi: Mienendo inayokinzana ya Marekani inazidisha kutoaminiwa diplomasia
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mienendo inayokinzana ya Marekani ndio sababu ya kuongezeka kutoaminiana katika uga wa diplomasia.
Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kusema bayana kwamba, kupigwa hatua katika mazungumzo kunahitaji azma na irada ya kweli kutoka upande wa pili.
Araghchi ameashiria utendaji wa kuwajibika wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuchagua njia ya kidiplomasia ya kutatua kadhia bandia iliyoundwa juu ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran na kubainisha kwamba, kuendeleza njia hii kunahitaji nia na uhalisia wa dhati kutoka upande wa pili.
Aidha katika mazungumzo hayo, Arghchi amemfahamisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na mwenendo wa mazungumzo yasiyo ya ana kwa na baina ya Iran na Marekani na hatua zilizopigwa katika mazungumzo hayo.
Katika upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi amesema, kurudia kila mara kauli za uwongo hakubadilishi ukweli wa kimsingi na kueleza bayana kwamba, Iran, ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizotia saini mkataba wa NPT, ina haki ya kumiliki mzunguko kamili wa fueli ya nyuklia.
Seyyed Abbas Araqchi ameeleza hayo katika ujumbe alioweka kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X na kubainisha: "mimi, kimsingi, naepuka kurusha hewani kupitia vyombo vya habari hoja zinazohusu vipengele muhimu vya mazungumzo ".
Hayo yanajiri katika hali ambayo, viongozi wa Iran waneendelea kusisitiza tena irada na azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutumia diplomasia kudhamini maslahi halali na ya kisheria ya wananchi wa Iran na kukomesha vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi ambayo yanakanyaga haki za binadamu na ustawi wa kila Muirani.