UNICEF: Watoto wa Gaza wanazidi kujongewa na njaa, maradhi na mauti
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeonya kwamba watoto katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na hatari kubwa ya njaa, magonjwa na vifo, miezi miwili baada ya kukabiliwa na mzingiro wa Israel.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell, katika taarifa yake inayoangazia hali ya watoto katika Ukanda wa Gaza baada ya miezi miwili ya vikwazo vya Israel na kunyimwa misaada ya kibinadamu.
Russell amesisitiza tena wito wake wa kuondolewa vizuizi huko Gaza, kuruhusu kuingia kwa bidhaa za biashara, kuachilia wafungwa, na kulinda watoto. "Kwa muda wa miezi miwili, watoto katika Ukanda wa Gaza wamekabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara, kunyimwa bidhaa muhimu, huduma muhimu na huduma za afya za kuokoa maisha. Kwa kila siku ambayo inapita chini ya vikwazo vya Israel kwa misaada, wanakabiliwa na hatari ya kuongezeka kwa njaa, magonjwa, na kifo. Hakuna kinachohalalisha hili," alisema.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, asasi mbalimbali za kimataifa zimeendelea kuonya kuhusiana na hali mbaya ya uhaba na ukosefu wa chakula katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa, hivi sasa maghala ya chakula katika ukanda huo yapo tupu.
Mashirika ya kimataifa hayo ya yametangaza kuwa, chakula chote katika Ukanda wa Gaza kimeisha, na kueleza kwamba, maafa ya kibinadamu katika Ukanda huo yamefikia kiwango cha maafa na sasa eneo hilo liko katika hatua ya njaa halisi.