Israel yaendeleza mauaji ya kikatili Ukanda wa Ghaza, Yemen yapiga tena
(last modified Sat, 03 May 2025 02:24:31 GMT )
May 03, 2025 02:24 UTC
  • Israel yaendeleza mauaji ya kikatili Ukanda wa Ghaza, Yemen yapiga tena

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, raia 12 wa Palestina wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kikatili ya Wazayuni kwenye maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Ghaza hususan katikati mwa ukanda huo. Ukatili huo ulianzia usiku wa manane jana na kuendelea mpaka asubuhi.

Wazayuni wavamizi wameendeleza ukatili wao kwa siku ya 47 leo Jumamosi huku kama kawaida wahanga wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto wadogo. 

Duru za Palestina zimeripoti kuwa, ndege za kivita za utawala huo ghasibu wa Kizayuni zimeshambulia kwa mabomu nyumba nyingine kadhaa katikati mwa Ukanda wa Ghaza na kuua shahidi raia kadhaa wasio na hatia na kujeruhi wengine wengi.

Duru za matibabu za Palestina zimetangaza kuwa raia 12 zaidi wasio na hatia wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kikatili ya Israel yanayoendelea huko Ghaza.

Kwa upande wake televisheni ya Al Jazeera imenukuu taarifa ya watu waliomo kwenye msafara wa meli za msaada za Freedom Flotilla wakisema kuwa Israel imeshambulia meli hizo kwa kutumia droni na kuzikwamisha zisiendelee na safari. 

Taarifa nyingine zinasema kwamba, jeshi la Israel limekiri kwamba maeneo ya kaskazini mwa Palestina (yaliyopachikwa jina bandia la Israel) yamepigwa kwa kombora kutoka Yemen. Ingawa jeshi hilo limedai kuwa limetungua kombora hilo, lakini madai yake hayajathibitishwa na duru za kuaminika.

Taarifa hizo zimesema kuwa ving'ora vya tahadhari vimesikika katika sehemu kubwa za maeneo la Galilaya, jimbo la Haifa na eneo la Wadi A'ra.

Ikumbukwe kuwa, wakati duru za Kizayuni zinapodai zimetungua makombora huwa zinafanya hivyo kujaribu kupunguza hasira za Wazayuni kwani mara nyingi zinakiri kuwa, zinaposema zimetungua hazina maana kwamba zimesambaratisha makombora hayo na kwamba sehemu kubwa sana ya makombora ya Yemen yanapiga maeneo yalikokusudiwa.