Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran apanga kuzuru Pakistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i125984-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_iran_apanga_kuzuru_pakistan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, anapanga kuzuru Pakistan na India wiki hii kama sehemu ya mashauriano yanayoendelea ya Tehran na nchi za kikanda huku kukiwa na mvutano baina ya nchi hizo mbili jirani.
(last modified 2025-05-04T11:33:20+00:00 )
May 04, 2025 11:33 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran apanga kuzuru Pakistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, anapanga kuzuru Pakistan na India wiki hii kama sehemu ya mashauriano yanayoendelea ya Tehran na nchi za kikanda huku kukiwa na mvutano baina ya nchi hizo mbili jirani.

Esmaeil Baghaei ameiambia Press TV siku ya Jumamosi kuwa Araghchi atawasili Pakistan Jumatatu kufanya mashauriano na maafisa wa ngazi za juu wa Pakistan.

Amesema mazungumzo hayo yatajikita katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kushughulikia maendeleo ya karibuni katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Baghaei pia amethibitisha kuwa mwanadiplomasia huyo mkuu atafanya ziara rasmi nchini India baadaye wiki hii.

Ziara hizo zimepangwa kufanyika wakati kukiwa na mvutano mkubwa kati ya nchi hizo mbili zenye silaha za nyuklia kuhusu shambulio la kigaidi la Aprili 22 katika eneo la Kashmir linalosimamiwa na India, ambalo liliua watu 26.India imelaumu Pakistan kwa shambulio hilo, lakini Pakistan imekanusha tuhuma hizo.

Katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi mnamo Aprili 26, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alilaani shambulio hilo na kusisitiza umuhimu wa mapambano ya pamoja dhidi ya ugaidi.

Katika simu nyingine na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif siku hiyo hiyo, Pezeshkian alieleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa mvutano kati ya India na Pakistan kufuatia shambulio hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia alizungumza kwa simu na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Muhammad Ishaq Dar, mnamo Aprili 26, ambapo alieleza utayari wa Tehran kusaidia kupunguza mvutano kati ya New Delhi na Islamabad.