Iran yalaani jinai za kivita za Marekani nchini Yemen
(last modified Sat, 03 May 2025 02:43:08 GMT )
May 03, 2025 02:43 UTC
  • Iran yalaani jinai za kivita za Marekani nchini Yemen

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei amelaani vikali wimbi la mashambulizi ya jeshi la Marekani katika muda wa saa 24 zilizopita katika maeneo mbalimbali ya majimbo ya Sana'a, Saada, na Al-Jawf nchini Yemen, yakilenga miundombinu na maeneo ya makazi ya Yemen.

Baqaei ametaja uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Yemen kuwa ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala Yemen na ukiukaji mkubwa wa kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kanuni na sheria za kimataifa.

Amesisitiza kuwa, mashambulizi hayo ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kwa sababu yanalenga maeneo ya makazi na miundombinu muhimu nchini Yemen.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameelezea masikitiko yake juu ya kutochukuliwa hatua Marekani na Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama katika kukabiliana na ukiukaji huo wa wazi wa sheria na mauaji ya watu wasio na hatia. Amebainisha kuwa, kuendelea uchokozi wa Marekani huko Yemen kunashadidisha ukosefu wa usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia, huku akizikumbusha nchi zote za eneo hili kuwa zina wajibu wa kukabiliana na jinai hizo za Marekani.

Katika hatua nyingine, mamia ya maelfu ya wananchi wa Yemen hapo jana walijitokeza katika barabara za mji mkuu Sana’a kushiriki maandamani ya kulaani mauaji ya kimbari huko Gaza na hujuma za Marekani dhidi ya nchi yao.

Malaki ya Wayemen katika maandamano ya kulaani jinai za US Gaza, Yemen

Waandamanaji hao walisema kuwa kwa kuunga mkono adui (Israel) na uchokozi wake dhidi ya Yemen, Marekani haiwezi kuzuia uungaji mkono wa Yemen kwa Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa Televisheni ya Al-Masirah, taarifa ya mwisho ya maandamano hayo, ambayo yalifanyika chini ya kaulimbiu 'Kusimama Imara katika Kuunga mkono Gaza na Palestina na Kukabiliana na Wauaji na Mabeberu', ilisema kuwa Vikosi vya Wanajeshi vya Yemen vimeisababishia hasara kubwa Marekani, na kwamba shambulio la hivi punde zaidi ni hujuma dhidi ya mnowari ya kubebea ndege ya Truman ya nchi hiyo.