Wanafunzi sita wasimamishwa masomo Marekani kwa kuunga mkono Palestina
(last modified Sun, 04 May 2025 02:36:38 GMT )
May 04, 2025 02:36 UTC
  • Wanafunzi sita wasimamishwa masomo Marekani kwa kuunga mkono Palestina

Katikati ya mvutano unaoongezeka katika chuo cha Swarthmore College huko Pennsylvania, Marekani wanafunzi sita wamesimamishwa masomo bila kupewa haki ya kusikilizwa kwa kuanzisha kambi ya kuunga mkono Palestina.

Kundi la Wanafunzi wa Haki kwa Palestina (Students for Justice in Palestine – SJP) wa Swarthmore limesema katika taarifa kwamba wanafunzi hao waliamriwa kuondoka katika eneo la chuo.

Kati ya wanafunzi hao sita waliosimamishwa, taarifa ilibainisha kuwa wanne ni watu wasiowazungu na wenye uwezo mdogo wa kifedha. Taarifa hiyo imesema: “Hii ni sehemu ya mwenendo wa kutisha wa Swarthmore kutumia udhaifu wa waandamanaji wanafunzi kwa misingi ya ubaguzi wa rangi."

Wanafunzi waliosimamishwa kwa muda wamezuiwa kuhudhuria shughuli yoyote ya chuo au hata kuingia katika eneo la chuo. Kwa mujibu wa SJP, hii ni mara ya kwanza kwa chuo hicho kusimamisha wanafunzi kwa kushiriki maandamano tangu angalau miaka ya 1960.

Rais wa Swarthmore College, Valerie Smith, alidai katika taarifa yake Alhamisi iliyyopita kwamba wanafunzi waliosimamishwa masomo waliharibu mali ya chuo.

Smith aliongeza kwamba wanafunzi hao walipuuza maagizo ya mara kwa mara ya kuondoka katika eneo la Trotter Lawn, ambako waliweka kambi yao ya kuunga mkono Palestina. 

Swarthmore College ni miongoni mwa taasisi nyingi za elimu ya juu Marekani ambazo zinachunguzwa na utawala wa Trump kwa madai ya kupunguza bajeti kutokana na harakati za kuunga mkono Palestina.

Licha ya hatua za kinidhamu zinazochukuliwa na utawala wa Trump, wanafunzi wanaoandamana kuitetea Palestina wamezindua kambi mpya katika vyuo na taasisi kadhaa za Marekani msimu huu, wakifufua harakati za mwaka jana za kupinga vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Tangu kuanza kwa vita hivyo tarehe 7 Oktoba 2023, angalau Wapalestina 52,400, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Mwezi uliopita, Chuo Kikuu cha Yale kilikumbwa na ukandamizaji wa maandamano ya mamia ya wanafunzi walioweka kambi, hatua iliyosababisha kusambaratishwa kwa maandamano hayo ndani ya siku chache na kukamatwa kwa wanafunzi 44, baadhi yao sasa wakikabiliwa na hatua za kinidhamu kutoka kwa chuo.

Tangu Januari, utawala wa Trump umekuwa ukikandamiza wanafunzi wanaoonyesha uungaji mkono na kushiriki katika maandamano ya kuunga mkono Palestina.