Watu 27 wauwawa baada RSF kuteka mji muhimu Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125946-watu_27_wauwawa_baada_rsf_kuteka_mji_muhimu_sudan
Watu wasiopungua 27 wameuawa baada ya kundi la wapiganaji wa vikosi vya RSF, linaloongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kuripotiwa kuwa limefanikiwa kuuteka mji wa kimkakati wa En Nahud nchini Sudan.
(last modified 2025-05-03T07:39:02+00:00 )
May 03, 2025 07:39 UTC
  • Watu 27 wauwawa baada RSF kuteka mji muhimu Sudan

Watu wasiopungua 27 wameuawa baada ya kundi la wapiganaji wa vikosi vya RSF, linaloongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kuripotiwa kuwa limefanikiwa kuuteka mji wa kimkakati wa En Nahud nchini Sudan.

Mji huo ni kituo muhimu kusini mwa jimbo la Kordofan magharibi unaotumiwa kuwapeleka wanajeshi Darfur magharibi mwa Sudan.

Kwa mujibu wa Shirika la kufuatilia haki za binadamu la Emergency Lawyers wapiganaji wa RSF, waliwakamata raia hao na kuwauwa likiwashutumu kwa kushirikiana na jeshi rasmi la Sudan.

Siku ya Ijumaa, kundi hilo lilitangaza kuwa wapiganaji wake wameuteka pia mji wa wa El Khoei ulio umbali wa kilomita 100 kutoka En Nahud. Mashuhuda wanasema kuwa, wanajeshi waliondoka kwenye eneo hilo na kuelekea katika mji mkuu wa jimbo la Kordofan Kaskazini.

Sudan imekuwa katika mgogoro mbaya wa vita vya uchu wa madaraka baina ya makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya Aprili 2023. Makadirio ya karibuni kabisa ya mashirika ya kimataifa yanasema kuwa, watu wasiopungua 30,000 wameshauawa tangu wakati huo na milioni 15 wengine wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.

Makamanda hasimu wa kijeshi nchini Sudan

 

Wakati huo huo, makumi ya maelfu ya Wasudani waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na vita sasa wanarejea nchini licha ya vita kuendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Sudan.

Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa baadhi ya raia wa Sudan wameanza taratibu kurudi nchini na kwamba idadi ya watu wanaorudi Sudan kutoka nchi jirani inaongezeka.  Wasudani wasiopungua milioni 1 na laki tano walikimbilia Misri mara baada ya kuibuka vita nchini kwao.