Ghasia dhidi ya wahamiaji Afrika Kusini zatarajiwa leo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139522-ghasia_dhidi_ya_wahamiaji_afrika_kusini_zatarajiwa_leo
Afrika Kusini inakabiliwa na mtihani mkubwa wa kiusalama baada ya magenge ya wahalifu kuapa kuwatimu raia wa kigeni nchini humo kuanzia leo.
(last modified 2026-06-30T03:45:14+00:00 )
Jun 30, 2026 03:42 UTC
  • Wahajiri wako hatarini Afrika Kusini
    Wahajiri wako hatarini Afrika Kusini

Afrika Kusini inakabiliwa na mtihani mkubwa wa kiusalama baada ya magenge ya wahalifu kuapa kuwatimu raia wa kigeni nchini humo kuanzia leo.

Magenge ya kujichukulia sheria mkononi (vigilante) yanayopinga wahamiaji, yanataka kufukuzwa nchini humo wahamiaji wasiokuwa na vibali halali na kuimarishwa udhibiti wa mipaka. Magenge hayo yalikuwa yamewapa raia wa kigeni hadi leo Juni 30 kuondoka nchini Afrika Kusini la sivyo watashambuliwa. Maandamano makubwa yanatarajiwa huku suala la uhamiaji likigeuka kuwa kisingizo kinachotumiwa na wananchi wanaokabiliwa na msururu wa changamoto za kijamii na kiuchumi.

Wanaopinga uhamiaji wamawalaumu raia wa kigeni kuwa “wanaiba ajira,” kuzidisha msongamano mashuleni na kuilemea sekta ya afya. Hata hivyo, kwa mujibu wa Sensa ya hivi karibuni ya Afrika Kusini (2022), wahamiaji wanaunda asilimia 4.1 tu ya wakazi wa nchi hiyo.

Wahamiaji kutoka Ghana, Nigeria na mataifa mengine wanasema wanashambuliwa bila kujali hadhi yao ya kisheria. Nchi kadhaa za kigeni zimeanza kuwaondoa raia wao nchini Afrika Kusini kama hatua ya tahadhari.

Kufuatia maandamano ya karibuni dhidi ya wahamiaji, serikali ilishughulikia zaidi ya raia wa kigeni 8,000 kwa ajili ya kurejeshwa makwao kupitia kituo cha mpakani cha Beitbridge katika kipindi cha chini ya wiki mbili.

Tangu wakati huo, Pretoria imetangaza mpango wa usalama wa rand milioni 600 (takribani dola milioni 36). Siku ya Jumanne itadhihirisha iwapo mpango huo utafanikiwa au nchi hiyo itatumbukia katika mgogoro mkubwa wa usalama.

Kwa muda mrefu, Afrika Kusini imekuwa kivutio kwa wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wanaotafuta maisha bora kutokana na uchumi wake imara.

Mapema mwezi uliopita, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, alimweleza mwenzake wa Kenya, Rais William Ruto, kwamba maandamano ya hivi karibuni dhidi ya uhamiaji haramu nchini humo hayamaanishi kuwa Waafrika Kusini wana chuki dhidi ya wageni huku akisisitiza kuwa wasiotakikana na wahamiaji haramu.