Kongo yamuondolea kinga Kabila ikimtuhumu kwa uhalifu wa kivita
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeanzisha mchakato wa kumuondolewa kinga Rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila ili aweze kukabiliwa na mashtaka ya kuunga mkono waasi wa M23 mashariki mwa nchi.
Waziri wa Sheria wa DRC, Constant Mutamba amewaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa kwamba, Mwanasheria Mkuu wa Jeshi la Kongo amelitaka Baraza la Seneti la Kongo kubatilisha kinga ya kutoshtakiwa ambayo Kabila anayo kama seneta katika maisha yake yote.
Kongo imekusanya ushahidi wa wazi wa "uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya raia wasio na hatia na wanajeshi," Mutamba amesema, akiongeza kuwa Kabila anapaswa kurejea Kongo kukabiliana na sheria au ahukumiwe bila kuwepo mahakamani.
Mwezi uliopita, serikali ya DRC ilisema imekisimamisha chama cha kisiasa cha Kabila, siku chache baada ya kuvamiwa kwa mali zake na vyombo vya usalama. Ilisema uamuzi huo ulichukuliwa kufuatia harakati za chuki zinazofanywa na Kabila ambaye aliwahi kuwa rais wa taifa hilo kwa miaka 18 hadi mwaka 2019.
Kabila bado ni kiongozi wa chama cha kisiasa cha Peoples Party for Reconstruction and Democracy PPRD. Taarifa hiyo pia iliweka wazi kwamba shughuli zote za chama hicho zimesimamishwa nchi nzima.
Rais wa sasa wa DRC, Felix Tshisekedi anamtuhumu Kabila kwamba anaandaa kile alichosema ni ''uasi '' na anaunga mkono muungano unaojumuisha kundi la M23 ambalo linaendesha vita dhidi ya vikosi vya serikali katika eneo la mashariki mwa nchi.
Haya yanaarifiwa huku Congo DR na Rwanda zikiahidi kuandaa rasimu ya makubaliano ya amani kufikia leo Mei 2, na kuacha kutoa msaada wa kijeshi kwa makundi yenye silaha, kwa mujibu wa makubaliano yaliyotiwa saini mjini Washington Aprili 25.