Basi lenye watu 70 lawaka moto Uganda, wengi wahofiwa kufa
(last modified Tue, 06 May 2025 10:58:37 GMT )
May 06, 2025 10:58 UTC
  • Basi lenye watu 70 lawaka moto Uganda, wengi wahofiwa kufa

Watu wengi wanahofiwa kufariki dunia baada ya basi la abiria kupinduka na kuwaka moto Jumatatu jioni katika wilaya ya Bukiwe ya katikati mwa Uganda.

Michael Kananura, msemaji wa Kurugenzi ya Usalama wa Barabarani amethibitisha habari hiyo kwenye taarifa yake maalumu na kusema kuwa, makumi ya watu wamepoteza maisha baada ya basi kugongana na bodaboda na baadaye kupinduka na kuwaka moto katika kituo cha biashara cha Makindu.

Kwa mujibu wa polisi, basi hilo lilikuwa likisafiri kutoka Kampala, mji mkuu, kuelekea wilaya ya mashariki ya Soroti. Ajali hiyo imetokea kando ya barabara kuu inayounganisha Kisoga na Nyega, yapata saa kumi na moja jioni kwa majira ya eneo hilo.

Kananura amesema: "Basi hilo limepinduka na kuwaka moto na kusababisha vifo vya watu. Tutaendelea kutoa taarifa mpya zaidi kadiri habari zitakavyokuwa zinatufikia."

Amesema abiria waliokuwa na majeraha mengi wamepelekwa haraka katika Hospitali ya Kawolo, Hospitali ya Mtakatifu Francis Lwanga wilayani Buikwe na kwenye vituo vingine vya afya vilivyoko karibu na eneo la ajali ili kupatiwa matibabu.

"Polisi na watoa huduma za dharura wapo eneo la tukio, wakifanya kazi ya kuzima moto huo na kuopoa miili ya walioapoteza maisha kwenye ajali hiyo," amesema Kananura.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamerusha picha na video kwenye mitandao ya kijamii huku vyombo vya habari nchini Uganda vikiripoti kuwa zaidi ya watu 40 wamepoteza maisha. Imeripotiwa kuwa, basi hilo lilikuwa na abiria 70 wakati ajali hiyo ilipotokea.