Watu saba wapoteza maisha katika mafuriko Mogadishu, Somalia
Watu wasiopungua saba wamefariki dunia na barabara kuu zimeharibiwa baada ya mvua kubwa kusababisha mafuriko katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, usiku wa Ijumaa kutokana na mfumo wa mifereji ya mvua kuzidiwa, na ongezeko la idadi ya watu mijini.
Msemaji wa serikali ya mkoa, Abdinasir Hirsi Idle, aliwaambia waandishi wa habari jana Jumamosi kuwa juhudi za uokoaji zilikuwa zinaendelea.
Amesema: “Idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwa sababu mvua zilikuwa kubwa na ziliendelea kwa masaa kadhaa na kubomoa nyumba tisa katika vitongoji kadhaa, na barabara kuu sita zimepatwa na uharibifu mkubwa.”
Somalia imekuwa ikikumbwa na mitikisiko mikali ya hali ya hewa ikiwemo misimu ya kiangazi mirefu ambayo imesababisha ukame na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko.
Mvua za Ijumaa ziliendelea kwa takriban masaa manane, zikiacha mafuriko yenye kina cha maji hadi kiunoni katika vitongoji ambako baadhi ya wakazi walikuwa wamekwama na wengine walilazimika kuhamia maeneo ya juu.
Mafuriko pia yaliharibu miundombinu muhimu, yakiwaacha wakazi bila usafiri wa umma na kusababisha usumbufu wa muda katika uendeshaji wa uwanja mkuu wa ndege, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Abdulle. Maafisa walithibitisha baadaye kuwa safari za ndege zilikuwa zinaendelea kama kawaida.
Shirika la Usimamizi wa Majanga la Somalia halijatoa taarifa rasmi ya vifo lakini lilisema tathmini inaendelea ili kubaini ukubwa wa uharibifu.
Wizara ya Nishati na Maji ya nchi hiyo ilisema katika taarifa yake Jumamosi kuwa, “mvua kubwa, zinazozidi milimita 115, zilirekodiwa kwa zaidi ya masaa 8 mfululizo” na ilitoa tahadhari kuhusu mafuriko ya ghafla katika maeneo mengine nje ya mji mkuu.