Misri yafurahia kurejeshwa turathi nyingi zilizoibwa na Marekani
(last modified Wed, 14 May 2025 02:45:12 GMT )
May 14, 2025 02:45 UTC
  • Misri yafurahia kurejeshwa turathi nyingi zilizoibwa na Marekani

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetangaza habari ya kurejeshwa nchini humo kutoka Marekani turathi 25 za kihistoria na za kisanii, zilizotwaliwa enzi za ustaarabu wa kale wa Misri.

Ubalozi mdogo wa Misri mjini New York ulisimamia urejeshwaji wa turathi hizo, ambazo Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeeleza kuwa ndicho kiasi kikubwa zaidi cha nyara za kale zilizosafirishwa kwa njia haramu na zilizopatikana katika siku za hivi karibuni.

Mkusanyiko huo unajumuisha vifuniko vya mawe na mbao vya sarcophagus, vinyago vya kauri na vilivyopambwa vya mbao vya 'mazishi,' chombo kikubwa cha alabasta, na mchoro wa mwanamke unaorejea nyuma hadi enzi ya Wagiriki na Warumi (baina ya miaka 332 Kabla ya Isa AS na 640 baada yake).

Vitu vingine vilivyopatikana pia ni aina mbalimbali za vito vilivyotengenezwa kwa madini mbalimbali ya chuma, sarafu ya dhahabu adimu kutoka enzi ya Ptolemy I, na sanamu dogo la shaba na mawe zinazoonyesha vipengele vya imani ya kale ya Misri na mila za kisanii.

Wananchi wa Misri wamesema kurejeshwa turathi hizo za thamani kutasaidia katika mchakato wa kupoza majeraha ya nafsi yaliyosababishwa na uporaji na jinai za wakoloni; na kukuza utalii wa nchi hiyo.

Nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikitaka kurejeshwa turathi na dafina zao za kale zilizoporwa na wakoloni wa Ulaya wakati wa kipindi cha ukoloni.  Weledi wa mambo wanatumai kuwa, maelfu ya turathi za kihistoria zilizoibiwa wa wakoloni barani Afrika katika enzi za ukoloni zitarejeshwa katika nchi zao za asili.