Magaidi wenye mfungamano na al-Qaeda waongeza mashambulio yao Msumbiji
Wanamgambo wanaoaminika kuwa wanachama wa kundi la kigaidi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa (ASWJ) lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda wameongeza mashambulio yao kaskazini mwa Msumbiji na kuzusha wasiwasi kwa mara nyingine.
Eneo la Kaskazini mwa Msumbiji linakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa magaidi. Wanamgambo hao wamedai kuhusika kwenye mitandao yake ya kijamii kwa mashambulizi mawili dhidi ya wanajeshi wa Msumbiji katika eneo la kaskazini la Cabo Delgado.
Idadi ya waliouawa ni askari zaidi ya thelathini. Tangu mwanzoni mwa mwezi Mei, magaidi hao wamekuwa wakiongeza mashabulizi yao katika eneo hili.
Kwenye mitandao yao ya kijamii, magaidi huonyesha vifaa ambavyo walipata kutoka kwa jeshi baada ya mashambulizi yao: safu nzima ya bunduki ndogo, makmbora, risasi, na hata taa za jua.
Mnamo Mei 27, wanajihadi walishambulia kambi ya kijeshi huko Macomia, karibu kilomita 200 kaskazini mwa Pemba, mji mkuu wa Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji. Walidai kuhusika na vifo vya wanajeshi kumi. Shambulio hili linakuja muda mfupi baada ya shambulio kwenye kituo cha jeshi huko Muidumbe, ambapo wanajeshi kumi na mmoja pia waliuawa.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, jeshi la Msumbiji lilitangaza mwezi uliopita wa Aprili kwamba, limedhibiti kambi za mwisho za mafunzo zilizokuwa zikitumiwa na waasi katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado, ikiwa ni ishara ya kile walichokitaja maafisa wa jeshi hilo kuwa ni kumalizika kwa uasi wa miaka mingi katika eneo hilo lenye utajiri wa maliasili ya gesi.
Kiwango kikubwa cha gesi asilia kiligunduliwa katika eneo la Cabo Delgado mwaka 2010. Wapiganaji wanaohusishwa na kundi la kigaidi la DAESH walianzisha uasi mkoani humo mwama 2017 na kusitisha uchimbaji wa gesi hiyo. Imeelezwa kuwa watu wapatao 5,800 wameuawa katika machafuko na mapigano yaliyosababishwa na kundi hilo.
Kampuni ya TotalEnergies, ambayo ilisitisha mradi huo mkubwa wa uchimbaji gesi baada ya mashambulizi ya 2021 ambapo watu kadhaa waliuawa, imetangaza kuwa mradi huo utaanza tena mwaka huu pale "amani na usalama" vitakaporejea huko Cabo Delgado.