Shambulio la droni la waasi wa RSF laua watu sita hospitalini Sudan
(last modified Sat, 31 May 2025 07:10:56 GMT )
May 31, 2025 07:10 UTC
  • Shambulio la droni la waasi wa RSF laua watu sita hospitalini Sudan

Vikosi vya kijeshi vya Rapid Support Forces (RSF) vya Sudan vililishambulia jiji la El-Obeid siku ya Ijumaa kwa kutumia droni, na kuua watu sita katika hospitali moja muhimu kusini mwa nchi, kwa mujibu wa vyanzo vya kitabibu na kijeshi.

“Kundi hilo la waasi lilirusha droni dhidi ya Hospitali ya Bima ya Jamii, likiwaua watu sita na kuwajeruhi wengine 12, huku likishambulia pia maeneo ya makazi kwa mizinga mizito,” chanzo cha jeshi kililiambia shirika la habari la AFP, na kuongeza kuwa mashambulizi hayo pia yaliathiri hospitali nyingine katikati mwa mji huo.

Chanzo cha kitabibu kutoka Hospitali Kuu ya El-Obeid—ambayo ni kituo kikuu cha afya mjini humo—kimethibitisha idadi hiyo ya waliopoteza maisha, na kusema kuwa Hospitali ya Bima ya Jamii ililazimika kufungwa “kutokana na uharibifu mkubwa uliosababishwa na shambulio hilo la droni.”

Mji wa El-Obeid ni wa kimkakati, na uko takribani kilomita 400 (maili 250) kusini magharibi mwa Khartoum, na pia ndiyo makao makuu ya jimbo la Kordofan Kaskazini. Kwa karibu miaka miwili,mji huo umekuwa chini ya mzingiro wa RSF hadi jeshi la serikali lilipofanikiwa kuvunja mzingiro huo mwezi Februari.

Tangu wakati huo, licha ya kushindwa katika baadhi ya maeneo kama Khartoum, RSF imeendelea kushambulia El-Obeid, ambao unabaki kuwa kiungo muhimu cha usambazaji wa vifaa vya kijeshi kuelekea magharibi, ambako mji wa Al-Fashir—mji mkuu wa jimbo la Darfur—ndio pekee unaosalia mikononi mwa serikali.

Katika wiki za hivi karibuni, mapigano makali yamekuwa yakiendelea kati ya RSF na jeshi kwenye barabara inayounganisha El-Obeid na Al-Fashir.

Alhamisi, RSF ilitangaza kuwa imelitwaa tena mji wa Al-Khoei, ulioko takribani kilomita 100 (maili 60) magharibi mwa El-Obeid, baada ya kuupoteza kwa jeshi mapema mwezi huu.

Vita kati ya jeshi la Sudan na waasi wa RSF vilivyoanza mwezi Aprili 2023, vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kuwafurusha takribani watu milioni 13 kutoka makwao.

Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa mzozo huo sasa umechochea janga kubwa zaidi la njaa na wakimbizi duniani.