Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko nchini Nigeria yaongezeka hadi 151
Idadi ya waliofariki dunia kutokana na mafuriko makubwa kwenye mji wa Mokwa, wa kaskazini-kati mwa Jimbo la Niger nchini Nigeria, imepanda na kufikia hadi 151.
Taarifa ya jana Jumamosi ya serikali za mitaa za mji huo imesema: "Takwimu za hivi karibuni kabisa zilizotolewa na Ibrahim Hussaini, msemaji wa Wakala wa Usimamizi wa Dharura wa Jimbo la Niger (NSEMA), kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Jumatano jioni na kuendelea hadi Alkhamisi zinaonesha kuwa, mvua hiyo imesababisha uharibifu mkubwa na kusomba nyumba na miundombinu ikiwa ni pamoja na barabara na madaraja mawili.
"Idadi ya sasa ya vifo ni 151. Watu 3,018 wamelazimika kuhama makazi yao, familia 503 na nyumba 265 zimeathiriwa na maafa haya," amesema msemaji huyo wa serikali ya mkoa wa Niger.
Mji wa Mokwa ni kiungo kikuu cha kibiashara kati ya wafanyabiashara wa kusini na wazalishaji wa mazao ya kilimo wa kaskazini mwa Nigeria. Kwa kuzingatia hayo tutaona kuwa, madhara ya mafuriko hayo kwa binadamu na kwa uchumi ni makubwa sana.
Wakala wa Taifa wa Kusimamia Mambo ya Dharura nchini Nigeria (NEMA) uliitisha mkutano wa washikadau Ijumaa katika Jimbo la Niger ili kushughulikia maafa hayo na kujiandaa mapema ili kupunguza madhara kwa wananchi. Kampeni hiyo imepewa jina la "Kuimarisha Ustahimilivu, Kuimarisha Maandalizi," na imewaleta pamoja maafisa wa usimamizi wa maafa na washirika wao ili kuweka mikakati ya muda mrefu ya kukabiliana na mafuriko ya mara kwa mara. Rais Bola Tinubu wa Nigeria ameiamuru NEMA na vikosi vya usalama kuimarisha shughuli za kutafuta wahanga na uokoaji katika jamii zilizoathiriwa.