Uganda yadondosha msaada wa chakula Sudan Kusini
Jeshi la Uganda limetangaza kuwa limefanya zoezi la kudondosha tani 600 za chakula muhimu kwa ajili ya wakazi wa maeneo kadhaa ya jimbo lililokumbwa na ghasia la Upper Nile huko Sudan Kusini.
Chris Magezi, kaimu msemaji wa jeshi la UPDF amesema kuwa, jeshi hilo limesafirisha kwa ndege misaada ya kibinadamu iliyotolewa na washirika wa kimataifa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juba nchini Sudan Kusini hadi maeneo yaliyoathirika sana katika kaunti za Ulang na Nasir.
Mwezi Machi, mapigano makali yalizuka mjini Nasir kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF) na Jeshi la White Army, kundi la wanamgambo ambalo serikali inadai ni la chama cha upinzani cha Sudan People's Liberation Movement-in-Opposition kinachoongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar. Machar kwa sasa yuko chini ya kifungo cha nyumbani kwenye mji mkuu, Juba.
“Katika siku chache zilizopita, jeshi letu la anga limerusha hewani msaada wa dharura wa chakula katika maeneo yaliyokumbwa na hali ngumu ambapo maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kwa sasa wanaishi katika mazingira ya njaa kufuatia kuzuka vurugu za kutumia silaha zilizoanza mapema mwaka huu,” amesema kaimu msemaji wa Jeshi la Uganda.
Mwezi Machi mwaka huu Uganda ilipeleka wanajeshi wake Sudan Kusini, ili kuisaidia serikali ya Rais Salva Kiir kuimarisha usalama baada ya kuzuka mapigano makali.
Chris Magezi amesema pia kuwa, hali ya usalama katika eneo kubwa la mji mkuu Juba tangu wakati huo, imetulia na imeruhusu ujumbe wa kigeni na shughuli za biashara kuanza tena.