Kiongozi mwandamizi wa Inkatha Freedom Party cha Afrika Kusini auawa kwa risasi
Kiongozi mwandamizi wa Inkatha Freedom Party (IFP) nchini Afrika Kusini ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu na ni Naibu Spika Bungeni, Petros Sithole, ameuawa kwa kupigwa risasi Jumamosi jioni mjini Johannesburg.
Msemaji wa IFP, Mkhulengwa amesema katika taarifa rasmi ya chama hicho kwamba: "IFP inatangaza kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa mheshimiwa Khethamabala Petros Sithole, 68, kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana huko Katlehong jioni ya leo (Jumamosi). Kwa sasa maelezo yaliyopo ni ya kugongana. Ni matarajio ya IFP kwamba vyombo vya sheria havitaachana na jitihada zozote za kumfikisha mahakamani yeyote aliyehusika na mauaji haya."
Chama hicho kilichoasisiwa na mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi Mangosuthu Buthelezi, kinaongozwa na Velenkosini Hlabisa, ambaye pia anatumikia taifa kama Waziri wa Utawala wa Ushirika na Masuala ya Kimila kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ya Afrika Kusini.
Katikati ya mwaka 2024, chama cha upinzani nchini Afrika Kusini cha Inkatha Freedom Party kilishirikiana na chama tawala cha African National Congress (ANC) kuunda serikali huko Afrika Kusini.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya uchaguzi wa Mei 29, 2024 na baada ya matokeo ya uchaguzi kuonesha kuwa hakuna chama kilichopata ushindi mutlaki wa kukiwezesha kuunda Serikali peke yake.
Chama cha IFP kilipata viti 17 katika bunge la taifa lenye viti 400. Chama tawala cha ANC kilipata viti 159 na kililazimika kushirikiana na chama cha IFP kuunda serikali ya umoja wa kitaifa GNU.