Wananchi wa Burundi kuwachagua wawakilishi wao wa Bunge Alkhamisi hii
Wakati huu wakikabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi, raia wa Burundi ingawa wamechoka lakini wanajiandaa kushiriki uchaguzi mkuu wa wabunge wa Juni 5 ambao umepoteza mvuto kwa kukosekana kwa washindani wa kweli.
Taarifa zaidi zinasema, zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya uchaguzi huo keshokutwa Alkhamisi, mrengo wa upinzani umelalamikia ukosefu wa mafuta, vitisho na kushambuliwa kwa wanaharakati na chama tawala cha CNDD FDD, kama baadhi ya maswala ambayo yameathiri kampeni za mrengo huo.
Patrick Nkurunziza Rais wa muungano wa Burundi Bwa bose, amesema wiki tatu za kampeni zimekuwa ngumu kwa vyama vya upinzani, tofauti na upande wa chama tawala, ambacho kimeendeleza kampeni kubwa bila kupungukiwa na rasilimali.
Hata hivyo wananchi wanachoshughulishwa nacho kwa sasa ni gharama ya juu ya maisha, hali ambayo imewafanya kutochangamkia uchaguzi huo wa Alkhamisi.
Wanadiplomasia wameelezea wasiwasi kuwa kwa hali ilivyo inaonekana matokeo ya uchaguzi huo tayari yamefahamika.
Ripoti zinaeleza kuwa, waandishi wa habari ambao wametumwa kufuatilia uchaguzi huo, hawataruhusiwa kuripoti matokeo tofaut na yale yatakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi (CENI) la sivyo watakabiliwa na kifungo cha kati ya miaka mitano hadi kumi jela.
Mbali na uchaguzi wa wabunge na wilaya wa Juni 5, Burundi itaandaa uchaguzi wa maseneta Julai 23 na uchaguzi wa ngazi ya vijiji Agosti 25 mwaka huu. Uchaguzi ujao wa rais utafanyika mwaka 2027.