HRW: Waasi wa M23 waliwaua raia mashariki mwa DRC mwezi Februari
Shirika moja kimataifa la kutetea haki za binadamu, limeripoti kuwa waasi wa M23 waliwaua kwa makusudi raia wasiopungua 21 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwezi Februari mwaka huu.
Katika ripoti iliyotolewa Jumanne, Human Rights Watch ilisema mauaji hayo yalifanyika kati ya Februari 22 na 23, huku ikiongeza kuwa huenda idadi halisi ya waliouawa ni kubwa zaidi, hasa katika mji wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini ambao uko chini ya udhibiti wa waasi hao tangu mwishoni mwa Januari.
Kwa mujibu wa mashahidi waliotajwa katika ripoti hiyo, waasi wa M23 waliwaua watu saba mnamo Februari 22, magharibi mwa kambi ya kijeshi ya Katindo ,kambi ya zamani ya jeshi la serikali.
“Utawala wa kikatili wa M23 ndani ya Goma umezalisha hofu kubwa miongoni mwa wale wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na serikali ya DRC,” alisema Clémentine de Montjoye, mtafiti mwandamizi wa HRW anayehusika na eneo la Maziwa Makuu.
Amesema: “Mauaji haya ya halaiki hayaonekani kuwa matendo ya wapiganaji waliopoteza mwelekeo, bali yanaashiria mkakati wa uongozi wa M23 wa kuimarisha mamlaka yao kwa njia yoyote ile.”
Wiki iliyopita, msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, alikanusha vikali tuhuma za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaodaiwa kufanyika katika vituo vya kizuizi vinavyoendeshwa na kundi hilo mashariki mwa Kongo. Alizitaja tuhuma hizo, zilizotolewa na Amnesty International, kuwa “propaganda ya kupotosha isiyo na msingi.”
Kwa sasa, kundi la M23 linadhibiti maeneo makubwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, yakiwemo miji mikuu ya majimbo hayo — Goma na Bukavu.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu takriban milioni moja wamelazimika kuyakimbia makazi yao tangu mwishoni mwa Januari, huku mapigano yakiendelea kuikumba sehemu hiyo ya Kongo yenye utajiri mkubwa wa madini muhimu yenye thamani ya mabilioni ya dola.
Tangu mwanzoni mwa Januari 2025, waasi wa M23 wamechukua udhibiti wa maeneo kadhaa ya mashariki mwa Kongo, ikiwa ni pamoja na miji ya Goma na Bukavu, na wanaendelea kusonga mbele. Viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wainaishutumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi hao, lakini serikali ya Rwanda inakanusha tuhuma hizo na kusema kwamba kundi hilo linafanya kazi chini ya himaya ya serikali ya Kinshasa.