Niger yazituhumu nchi za Magharibi kwa njama za kuvuruga utawala wake
Rais wa mpito wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tchiani, amezituhumu nchi za Magharibi, hasa Ufaransa, kwa kuchochea machafuko ya kigaidi nchini humo kama njia ya kujaribu kulazimisha “mfumo mpya wa utawala” kinyume na matakwa ya raia wa Niger.
Katika mahojiano aliyofanya mwishoni mwa wiki na kituo cha televisheni ya taifa cha RTN, Jenerali Tchiani alidai kuwa “njama kadhaa” zimeanzishwa dhidi ya Niger kutoka nchi jirani kama Nigeria na Benin, zikisaidiwa na mabaki ya waliokuwa katika serikali za Magharibi zilizofukuzwa nchini humo baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Julai 2023.
Amesema mamluki wanaoungwa mkono na mataifa ya Magharibi wamekuwa wakikutana Nigeria na katika eneo la Ziwa Chad ili kuratibu juhudi za kuvuruga usalama, ikiwa ni pamoja na kusafirisha silaha kwa makundi ya kigaidi.
Ameongeza kuwa, Ufaransa imetumia mbinu mbalimbali kuvuruga Niger. Aidha, amesema kuwa serikali ya Paris imeunda " mitandao ya Kifaransa” katika ukanda wa Afrika Magharibi , mmoja ukiwa inaongozwa na Jean-Marie Bockel, mjumbe maalum wa Rais Emmanuel Macron kwa masuala ya Afrika, aliyekabidhiwa jukumu la kupinga “kueneza ushawishi wa Ufaransa eneo la Sahel.”
Kwa mujibu wa Tchiani, mtandao maalumu wa kuvuruga usalama eneo la Sahel na kwamba mtandao huo unahusishwa na idara ya ujasusi ya Ufaransa (DGSE), wanadiplomasia, na shirika la Francophonie, wakifadhiliwa kwa “raslimali zisizo na kikomo” ili kutekeleza oparesheni zote za “kivuruga” zinazolenga kuyumbisha Muungano wa Nchi za Sahel (AES). Muungano huo unazileta pamoja Mali, Burkina Faso na Niger.
Ameongeza kuwa hii pia imelenga kwa kila hali kuharibu uhusiano kati ya nchi wanachama wa Muungano wa Nchi za Sahel na Russia.
Hii si mara ya kwanza kwa Tchiani kutoa tuhuma kama hizo. Mnamo Desemba, alisema kuwa Ufaransa ilikuwa inafadhili waasi wanaofanya shughuli zao kuvuruga usalama katika majimbo ya Sokoto, Zamfara na Kebbi nchini Nigeria, pamoja na nchini Benin, kwa lengo la kudhoofisha mamlaka ya Niger. Alimtuhumu pia aliyekuwa mkuu wa ujasusi wa Nigeria, Ahmed Abubakar Rufai, kwa kuyapa makundi hayo mafunzo na vifaa.
Mnamo Januari, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger, Mohamed Toumba, naye aliishutumu Ufaransa kwa kutumia mbinu za siri kudhoofisha utawala wa kijeshi mjini Niamey.
Kwa upande mwingine, Russia, ambayo Niger, Mali na Burkina Faso zimegeukia kwa ushirikiano wa kiusalama miezi ya hivi karibuni imeunga mkono hoja za Niger, ikidai kuwa baadhi ya nchi za Magharibi zinafanya jitihada za makusudi kuyumbisha ukanda wa Sahel. Wiki iliyopita, afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Tatyana Dovgalenko, alituhumu Ukraine kwa kusambaza silaha kutoka nchi za Magharibi kwa makundi ya waasi barani Afrika, na kufundisha mitandao ya kigaidi katika Sahel kama sehemu ya “mkakati wa kuvuruga bara lote la Afrika.”