Wanajeshi wa Algeria waangamiza magaidi karibu na mpaka wa Tunisia
(last modified Wed, 04 Jun 2025 13:12:21 GMT )
Jun 04, 2025 13:12 UTC
  • Wanajeshi wa Algeria waangamiza magaidi karibu na mpaka wa Tunisia

Wizara ya Ulinzi ya Algeria imetangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeangamiza magaidi wawili wenye silaha katika operesheni inayoendelea ya kukabiliana na magenge ya kigaidi katika mkoa wa mashariki wa Khenchela, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Tunisia.

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, operesheni hiyo imefanyika katika eneo la Oued Boudhkane, takriban kilomita 500 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Algiers. Wanajeshi wamekamata bunduki mbili aina ya Kalashnikov na risasi kwenye eneo la tukio.

Wizara hiyo imeongeza kuwa, operesheni hiyo inaonesha kwamba hatari za kuzuka upya vitendo vya kigaidi ndani ya Algeria bado ipo lakini vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo viko macho na vimeazimia kikweli kuwasaka na kuwasafisha kabisa magaidi waliosalia.

Tukio hilo ni sehemu ya operesheni zinazoendelea za kijeshi zinazolenga kuyafuta magenge ya kigaidi katika majimbo ya kaskazini mwa Algeria. Mwezi Mei 2025, magaidi wawili waliuawa katika operesheni sawa na hii ya huko Khenchela, na wengine wawili waliuawa mwezi Julai 2024.

Wanajeshi wa Algeria mara kwa mara hufanya operesheni za kufagia magenge ya kigaidi katika maeneo ya milimani na vijijini, ambako mabaki ya vikundi vyenye misimamo mikali vinavyohusishwa na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda au Daesh (ISIS) hujikusanya na kujaribu kujipenyeza katika miji ya karibu.