UN yataka uchunguzi wa makaburi ya halaiki yaliyogunduliwa Libya
(last modified Thu, 05 Jun 2025 06:53:37 GMT )
Jun 05, 2025 06:53 UTC
  • UN yataka uchunguzi wa makaburi ya halaiki yaliyogunduliwa Libya

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kufanyika uchunguzi huru na wa kina, baada ya kugunduliwa makaburi ya halaiki katika jela na vituo vya kuzuilia watu nchini Libya.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu imesema "imeshtushwa" na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofichuliwa katika vituo rasmi na visivyo rasmi vya kuzuilia watu vinavyoendeshwa na wanamgambo wanaojulikana kwa jina la "Stabilization Support Apparatus (SSA)", viungani mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Haya yanajiri wiki chache baada ya mapigano makali kuzuka huko Tripoli kati ya vikosi vinavyomtii Waziri Mkuu Abdul-Hamed Dbeibah, ikiwa ni pamoja na Brigedi ya 444, na kundi lenye nguvu la wanamgambo wenye uhusiano na Baraza la SSA baada ya kuenea taarifa za kuuawa mkuu wa SSA, Abdul Ghani al-Kikli, anayejulikana kwa jina maarufu la "Ghaniwa."

Mei 19,  miili 58 ya watu ambao hawajulikani, ilipatikana katika hospitali moja mjini Tripoli iliyokuwa inadhibitiwa na wanamgambo hao wa SSA.

Umoja wa Afrika hivi karibuni ulielezea wasiwasi wake kuhusu mapigano makali kati ya makundi yenye silaha katika mji mkuu wa Libya Tripoli, ukitaka kusitishwa mara moja ghasia na umwagaji damu.

Ikumbukwe kuwa, Februari mwaka huu, mamlaka za Libya ziligundua miili ipatayo 50 kwenye makaburi mawili ya halaiki katika jangwa la kusini mashariki mwa nchi hiyo, katika maafa mengine yaliyohusisha watu wanaotaka kufika Ulaya kupitia nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.