Uchaguzi wa Bunge wafanyika Burundi, chama tawala chatarajiwa kuibuka na ushindi
Wapiga kura nchini Burundi leo wameelekea katika vituo vya kupiga kura huku kukiwa na ongezeko la mfumuko wa bei, uhaba wa mafuta na malalamiko ya ukandamizaji wa kisiasa.
Viti katika Bunge la Kitaifa na mabaraza ya mitaa vinawaniwa lakini Évariste Ndayishimiye yuko salama katika nafasi yake kama rais kwa kuwa anahudumu kwa muhula wa miaka saba unaomalizika 2027.
Uchaguzi huo utapima umaarufu wa chama tawala cha CNDD-FDD, kikundi cha waasi cha zamani ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 20 iliyopita.
Taifa hilo la Afrika Mashariki tayari ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, lakini wakazi wa huko wamewekewa shinikizo zaidi na ongezeko la bei ya bidhaa kama vile chakula hivi karibuni.
Vyama vya upinzani vimelalamika kuwa wafuasi wao wamekuwa wakinyanyaswa na kutishwa na wanachama wa vuguvugu la vijana wa CNDD-FDD, Imbonerakure.
Gabriel Banzawitonde, kiongozi wa chama cha APDR, alisema: ''Watu wanaogopa sana hadi wanakuambia hawawezi kuvaa rangi za chama chochote isipokuwa zile za chama tawala'.
Wanadiplomasia wameelezea wasiwasi kuwa kwa hali ilivyo inaonekana matokeo ya uchaguzi huo tayari yamefahamika.
Ripoti zinaeleza kuwa, waandishi wa habari ambao wametumwa kufuatilia uchaguzi huo, hawataruhusiwa kuripoti matokeo tofaut na yale yatakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi (CENI) la sivyo watakabiliwa na kifungo cha kati ya miaka mitano hadi kumi jela.
Mbali na uchaguzi wa wabunge na wilaya wa Juni 5, Burundi itaandaa uchaguzi wa maseneta Julai 23 na uchaguzi wa ngazi ya vijiji Agosti 25 mwaka huu. Uchaguzi ujao wa rais utafanyika mwaka 2027.