Rais wa Afrika Kusini: Mazungumzo ya kitaifa yataendelea bila mshirika wa muungano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127924-rais_wa_afrika_kusini_mazungumzo_ya_kitaifa_yataendelea_bila_mshirika_wa_muungano
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema kuwa mazungumzo ya kitaifa yenye lengo la kuimarisha umoja na kuiunganisha nchi baada ya uchaguzi wa mwaka jana yataendelea bila mshirika mkuu katika serikali ya mseto ya nchi hiyo.
(last modified 2025-07-04T15:19:03+00:00 )
Jul 04, 2025 15:19 UTC
  • Cyril Ramaphosa
    Cyril Ramaphosa

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema kuwa mazungumzo ya kitaifa yenye lengo la kuimarisha umoja na kuiunganisha nchi baada ya uchaguzi wa mwaka jana yataendelea bila mshirika mkuu katika serikali ya mseto ya nchi hiyo.

Chama cha Democratic Alliance (DA), chama kikubwa katika serikali ya muungao ya Afrika Kusini baada ya chama Africa National Congress kinachoongoza na Ramaphosa, wiki jana kilijitoa katika mazungumzo ya kitaifa baada ya Ramaphosa kumfuta kazi Naibu Waziri kutoka chama hicho. 

Mazungumzo ya kitaifa ya Afrika Kusini ni mchakato ulioanzishwa na Rais Ramaphosa ili kuiunganisha nchi hiyo baada ya uchaguzi wa mwaka jana, ambapo chama chake cha African National Congress (ANC) kilipoteza viti vingi vya uwakilishi bungeni kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo mitatu, hivyo kulazimika kuungana na chama cha DA kuunda serikali.

Vyama hivyo vimekuwa vikizozana mara kwa mara tangu muungano huo ulipoanzishwa mwaka mmoja uliopita, huku chama cha DA kikikihutumu chama cha ANC kuwa kinachukua hatua za upande mmoja.

Alipoulizwa katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa chama cha Democratic Alliance kujitoa katika mazungumzo ya kitaifa, Rais wa Afrika Kusini amesema: Tunataraji tutakuwa na mazungumzo chanya bila ya mijadala au kuingiliwa na chama ambacho hakina maslahi kwa watu wa Afrika Kusini.