Umoja wa Mataifa 'washtushwa' na mauaji ya waandamanaji Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128088
Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi mkubwa juu ya vifo vya watu zaidi ya 10 nchini Kenya, ambapo polisi na waandamanaji walikabiliana wakati wa maandamano ya kupinga sera za serikali ya nchi hiyo Jumatatu.
(last modified 2025-07-09T02:38:27+00:00 )
Jul 08, 2025 14:20 UTC
  • Umoja wa Mataifa 'washtushwa' na mauaji ya waandamanaji Kenya

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi mkubwa juu ya vifo vya watu zaidi ya 10 nchini Kenya, ambapo polisi na waandamanaji walikabiliana wakati wa maandamano ya kupinga sera za serikali ya nchi hiyo Jumatatu.

"Tumesikitishwa sana na mauaji ya jana ya watu 10, pamoja na uporaji na uharibifu wa mali nchini Kenya," Msemaji wa Ofisi ya Haki ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani aliwaambia waandishi wa habari huko Geneva jana Jumanne.

Amesema kuwa, "risasi hai, risasi za mpira, mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha yalitumika" wakati polisi wakiyakabili maandamano hayo." 

Afisa huyo mwandamizi wa haki za binadamu wa UN amesisitiza kwamba, polisi wa Kenya walikuwa wameripoti kwamba takriban watu 11 waliuawa, maafisa wa polisi 52 walijeruhiwa na 567 kukamatwa.

Aidha amenukuu takwimu za Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya, ambayo iliripoti vifo vya watu 10, majeruhi 29, kukamatwa watu 37 huku kadhaa wakitekwa nyara. Baadhi ya duru huru zimesema waliouawa katika maandamano ya Jumatatu wanapindukia watu 20

Maandamano hayo ya Saba Saba ya juzi Jumatatu yaliyoshirikisha maelfu ya watu yalikuwa ya kuadhimisha mapambano ya kudai demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya ya Julai 7, 1990, lakini yalichanganyika pia na miito ya kumtaka Rais William Ruto ajiuzulu.

Yakiwa yamechochewa na ugumu wa maisha, ukatili wa polisi, na msururu wa mauaji ya watu wakiwa chini ya ulinzi wa polisi, maandamano hayo yaliratibiwa na tabaka la vijana wa nchi hiyo almaarufu Gen Z.