Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Abdulhalim aaga dunia, amezikwa leo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128158-kadhi_mkuu_wa_kenya_sheikh_abdulhalim_aaga_dunia_amezikwa_leo
Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Abdulhalim Hussein Athman amefariki dunia usiku wa manane wa kuamkia leo mjini Mombasa na maziko yake yamefanyika leo.
(last modified 2025-07-10T13:17:28+00:00 )
Jul 10, 2025 13:13 UTC
  • Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Abdulhalim aaga dunia, amezikwa leo

Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Abdulhalim Hussein Athman amefariki dunia usiku wa manane wa kuamkia leo mjini Mombasa na maziko yake yamefanyika leo.

Kwa mujibu wa wanafamilia, Sheikh Abdulhalim, ambaye ni baba wa watoto watatu, alikuwa akiugua.

Mwaka 2024, Sheikh Abdulhalim alisafirishwa na kupelekwa nchini India kwa matibabu, ambapo alipata nafuu hadi akarudi Kenya kuendelea kuhudumu nafasi yake ya Ukadhi Mkuu.

Al Marhum Sheikh Abdulhalim ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 55 aliteuliwa kuwa Kadhi Mkuu Julai 17, 2023, na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), kuhchukua nafasi iliyoachwa wazi na Sheikh Ahmed Muhdhar aliyestaafu Disemba 2022 na kuwa Kadhi Mkuu wa 12 nchini Kenya.

Kabla ya kuteuliwa kwake, alikuwa akihudumu kama Kadhi Mkuu Msaidizi wa Nairobi, na pia aliwahi kuhudumu katika maeneo ya Kwale, Mombasa na Isiolo.

Alisomea Sheria za Kiislamu katika Chuo Kikuu maarufu cha Al-Azhar nchini Misri, na alipata mafunzo  maalumu ya mahakama nchini Saudi Arabia.

Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Kadhi Mkuu, Abdulhalim Athman Hussein na kusema kifo kimeipokonya Kenya mtu muhimu.

“Sheikh Abdulhalim Hussein Athman alitumikia mahakama na Wakenya kwa bidii, uwajibikaji, unyenyekevu na uadilifu,” ameasema Bi Koome katika ujumbe wake huo.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wanahabari Waislamu nchini Kenya MMPK Juma Namlola na Katibu Mshirikishi wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu Nchini (CIPK) tawi la Lamu, Bw Mohamed Abdulkadir ni miongoni mwa shakhsia wengine waliotuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Sheikh Abdulhalim wakimtaja kuwa ni kiongozi mcha Mungu, mwenye hekima na mwenye kujitolea kwa hali na mali katika kuongoza Mahakama za Kadhi na kuimarisha uelewa wa sheria za Kiislamu nchini Kenya.../