Mufti wa Misri alaani ziara ya ‘mashekhe wa Ulaya’ waliotembelea Israel
Mufti wa Misri, Sheikh Nazir Ayad, amelaani ziara iliyofanywa na kundi alilolitaja kama "wale wanaojitangaza kuwa shakhsia wa kidini", waliotembelea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel na kuitaja ziara hiyo kuwa ni "uwekezaji wa bei rahisi wa kisiasa kwa kutumia majoho bandia ya ushekhe ili kuipamba sura ya utawala ghasibu wa umwagaji damu".
Katika taarifa kali aliyotoa, Sheikh Ayad ameipinga ziara ya wajumbe hao iliyofanyika siku chache zilizopita na kukosolewa vikali pia na chombo cha juu zaidi cha kidini nchini Misri cha al-Azhar.
Taarifa yake inafuatia tangazo lilitolewa siku ya Jumatatu na ofisi ya Rais wa utawala kizayuni wa Israel Isaac Herzog, ambayo ilisema Herzog amewapokea katika ofisi yake ya Baitul Muqaddas Magharibi "maimamu na viongozi kutoka jamii ya Waislamu wa Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi, Italia na Uingereza".
Kwa mujibu wa ofisi ya Herzog, ujumbe huo uliongozwa na Hassen Chalghoumi na ulijumuisha iliowaita “watu mashuhuri wa Kiislamu waliokwenda Israel kutangaza ujumbe wa amani, kuishi pamoja na ushirikiano kati ya Waislamu na Wayahudi, na kati ya Israel na Ulimwengu wa Kiislamu.”
Mufti wa Misri ameeleza katika taarifa yake:
“Nimefuatilia kwa masikitiko makubwa ziara hii ya kufedhehesha iliyofanywa na kundi linalojitangaza kuwa watu mashuhuri wa kidini—watu ambao wameuza dhamiri zao kwa bei rahisi, na kujivika kibandia vazi la kidini, na kusimama mbele ya viongozi wa kundi la Kizayuni kwa namna ya kuaibisha”.
Ayad ameendelea kulishutumu kundi hilo akisema limehamasisha: "amani ya uwongo na mazungumzo yenye doa la damu za watu wasio na hatia", na kuongeza kwamba watu hao wanazungumzia kuishi pamoja na kufanya mazungumzo na wale ambao "hawajui falsafa ya kuishi pamoja wala lugha ya mazungumzo".../