Raila Odinga: Sikufaidika na hendisheki ya Uhuru Kenyatta
Kiongozi wa chama cha ODM nchini Kenya, Bwana Raila Odinga amepuuza madai yanayosema kuwa alinufaika kutokana na ushirikiano kati yake na Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta, akisema hakupewa nafasi yoyote serikalini au kupata manufaa ya kibinafsi.
Odinga amekanusha dhana kuwa alishiriki handisheki na Uhuru Kenyatta mwaka 2018 kwa nia ya kujitajirisha, akisema malengo yao yalikuwa kushinikiza mageuzi.
Waziri huyo mkuu wa zamani amesisitiza kuwa hakuna manufaa yoyote aliyopata kibinafsi au kupitia wandani wake kwenye serikali ya handisheki kama inavyodaiwa.
“Sikufaulisha uteuzi wa mtu yeyote kwenye serikali ya Uhuru. Nilipata nini? Sikupata chochote,” amesema Bw Odinga katika mahojiano.
Amesema ‘handisheki’ iliyozaa Jopo la Maridhiano (BBI) ililenga tu kushughulikia masuala ya uongozi na uwazi wakati wa uchaguzi mkuu.
Amesisitiza kuwa kutofaulu kwa BBI ndiko kulikochangia uchaguzi wa 2022 usiwe na uwazi na pia mgawanyiko ulioshuhudiwa kati ya makamishina wa Tume ya Uchaguzi (IEBC).
Bwana Odinga pia amekosoa uamuzi wa Mahakama ya Juu chini ya uongozi wa Jaji Martha Koome ambao ulidumisha ushindi wa Rais William Ruto, akisema haukuzingatia sheria.
Matamshi ya Odinga yanakuja baada ya kufufuliwa mjadala kuhusu handisheki ya 2018 baina yake na rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, uhalali wa kura za uchaguzii wa rais 2022 na ushirikiano wake wa sasa na Rais William Ruto kwenye Serikali Jumuishi.