Marais wawili wa zamani ni miongoni mwa wanaowania urais Malawi
Wagombea zaidi ya 20 nchini Malawi, wakiwemo marais wawili wa zamani, ni miongoni mwa wanasiasa wanaowania kiti cha urais katika uchaguzi ujao.
Ripoti zinasema marais hao wa zamani ni miongoni mwa waliorejesha fomu kwa Tume ya Uchaguzi nchini humo kuomba kuteuliwa kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba kuchuana na Rais Lazarus Chakwera.
Rais wa sasa Lazarus Chakwera, anayewania kwa muhula mwengine kupitia tiketi ya chama tawala Congress, anatarajiwa kuwasilisha fomu zake kwa Tume ya Uchaguzi Julai 30.
Katika kinyanganyiro hicho yumo pia rais wa zamani Peter Mutharika wa chama cha Democratic Progessive na Joyce Banda anayewania kwa tiketi ya chama cha Peoples.
Dalisto Kabambe gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Malawi naye pia yumo kwenye orodha ya wagombea hao. Mchakato wa kurejesha fomu ulianza rasmi jana Alkhamisi na unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi huu.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Uchaguzi, Joyce Banda atakuwa wa kwanza kuwasilisha fomu zake leo Ijumaa na atafuatiwa na Peter Mutharika.
Wagombea wengine kwenye uchaguzi huo ikiwa wataidhinishwa na tume ni pamoja na makamu wake wa sasa Michaeli Usi, makamu wa rais wa zamani Cassim Chilumpha pamoja na Atupele Muluzi ambaye ni mtoto wa rais wa zamani, Bakili Muluzi.