Wasudani zaidi ya milioni 1.3 waliokimbia makazi yao wamerejea nyumbani
Licha ya mzozo unaoendelea kote Sudan, zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni moja waliokimbia vita wamerejea katika makazi yao, pamoja na wengine 320,000 waliorejea nchini wakitokea Misri na Sudan Kusini tangu waliopata hifadhi katika nchi hizo mwaka jana.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limeripoti kuwa aghalabu ya raia hao wa Sudan wanarejea katika makazi huko Khartoum, Sennar na al Jazira mikoa ambayo imeathirika kwa vita kwa zaidi ya miaka miwili.
Taarifa ya shirika la UNHCR imeeleza kuwa: Licha ya mapigano kupungua katika maeneo hayo matatu, lakini si shwari huku njia za usambazaji wa umeme, barabara na mifumo ya mifereji ya maji ikiwa imeharibiwa kabisa, na shule na hospitali zimeathiriwa na vita au kugeuzwa kuwa makazi ya pamoja ya kuhifadhi familia zilizohamishwa.
Mamadou Dian Balde Mratibu wa Kikanda wa Wakimbizi katika mgogoro wa Sudan amesema kuwa: UNHCR na Wakurugenzi wa kanda wa Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) hivi karibuni waliitembelea Khartoum, ambapo walikuta maelfu ya watu waliokimbia makazi yao wamekatiwa misaada tangu vita vilipoanza.
Naye Othman Belbeisi Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) amesisitiza kuwa ipo haja ya kuwaunga mkono na kuwasaidia raia wa Sudan kurejea nyumbani kwa hiari.
Mahitaji ya kibinadamu ndani ya Sudan na katika nchi jirani zinazowahifadhi bado hayafikia kiwango kinachohitajika, huku mashirika ya misaada yakipokea tu asilimia 23 tu kati ya dola bilioni 4.2 zinazohitajika kwa ajili ya operesheni za kibidamu ndani ya Sudan na asilimia 16 tu ya dola bilioni 1.8 zinazohitajika kusaidia wakimbizi wa Sudan walioko nje ya nchi.