Magaidi 18 wa Al Shabaab waangamizwa katika mapigano makali Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128768
Magaidi wasiopungua 18 wa kundi la Al Shabaab waangamizwa nchini Somalia katika mapigano makali baina yao na jeshi la nchi hiyo likishirikana na askari wa Umoja wa Afrika.
(last modified 2025-07-26T07:39:46+00:00 )
Jul 26, 2025 07:39 UTC
  • Magaidi 18 wa Al Shabaab waangamizwa katika mapigano makali Somalia

Magaidi wasiopungua 18 wa kundi la Al Shabaab waangamizwa nchini Somalia katika mapigano makali baina yao na jeshi la nchi hiyo likishirikana na askari wa Umoja wa Afrika.

Aidha wanajeshi wanne wa Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) wameuawa na wengine saba kujeruhiwa kufuatia mapigano na kundi hilo la kigaidi siku ya Ijumaa, baada ya shambulio la kundi hilo kukabiliwa vikali na jeshi la Somalia likisaidiwa na wanajeshi wa Umoja wa Afrika waliopo nchini, katika eneo la Shabelle ya Chini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Somalia, Jeshi la Kitaifa la Somalia kwa kushirikiana na Kikosi cha Ulinzi cha Wananchi wa Uganda (UPDF)—ambacho ni sehemu ya Kikosi cha Umoja wa Afrika cha Usaidizi na Uimarishaji wa Amani Somalia (AUSSOM)—walifanikiwa kukabiliana na shambulio la al-Shabaab katika maeneo ya Sabiib na Canoole, na kuwaua magaidi 18.

Taarifa hiyo ilisema: “Vikosi vya taifa, ambavyo vilikuwa katika hali ya tahadhari na vimejiandaa kikamilifu, vilijibu haraka na kwa mafanikio shambulio hilo, na kufanikiwa kuvuruga jaribio la magaidi kuingia katika maeneo hayo.”

Wizara hiyo ilithibitisha kuwa wanajeshi wanne wa SNA waliuawa na wengine saba walijeruhiwa katika mapigano hayo, huku ikieleza kuwa msaada muhimu ulitolewa na washirika wa kimataifa wa usalama kupitia mashambulizi ya anga yaliyosababisha hasara kubwa kwa magaidi wa al-Shabaab.

Mapigano haya ni mwendelezo wa juhudi za hivi karibuni ambapo, kufuatia karibu miezi miwili ya mapigano ya mara kwa mara, jeshi la Somalia kwa msaada wa askari wa Umoja wa Afrika lilifanikiwa kurejesha vijiji vya kimkakati vya Anole na Sabid kutoka mikononi mwa al-Shabaab mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Vijiji vya Anole na Sabid, vilivyoko katika jimbo la kusini magharibi la Shabelle ya Chini, vina umuhimu wa kijeshi na kimkakati kwa kuwa ni sehemu ya njia kuu ya mawasiliano na usafirishaji katika eneo hilo.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limekuwa likiendesha uasi dhidi ya serikali ya Somalia kwa zaidi ya miaka 16, na mara kwa mara hushambulia vikosi vya usalama, maafisa wa serikali na raia wa kawaida.