Araghchi: Iran haitalegeza msimamo wake kuhusu mpango wa nyuklia wa amani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128750-araghchi_iran_haitalegeza_msimamo_wake_kuhusu_mpango_wa_nyuklia_wa_amani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesisitiza tena msimamo thabiti wa Tehran kuhusu haki yake ya kuendeleza mpango wake wa nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani, ikiwa ni pamoja na kurutubisha urani.
(last modified 2025-07-25T07:27:50+00:00 )
Jul 25, 2025 07:27 UTC
  • Araghchi: Iran haitalegeza msimamo wake kuhusu mpango wa nyuklia wa amani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesisitiza tena msimamo thabiti wa Tehran kuhusu haki yake ya kuendeleza mpango wake wa nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani, ikiwa ni pamoja na kurutubisha urani.

Akizungumza siku ya Alhamisi jijini Tehran, katika kikao na familia ya Meja Jenerali Mohammad Bagheri, aliyeuawa shahidi katika mashambulizi ya kichokozi ya Israel dhidi ya Iran,  kabla ya kuanza kwa duru ya sita ya mazungumzo kati ya Iran na nchi za Ulaya, Araghchi amesema:

“Ulimwengu unapaswa kufahamu kuwa tutaendelea kusimama kidete kutetea haki za wananchi wa Iran kuhusu matumizi ya nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani, hasa suala la urutubishaji wa urani.”

Aliongeza kuwa kufuatia hujuma ya karibuni ya pamoja kati ya Marekani na Israel tarehe 13 Juni,  ambayo ilisababisha vifo vya makamanda wa kijeshi wa Iran wakiwemo Jenerali Bagheri, pamoja na wanasayansi na raia wa kawaida , ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kutambua msimamo usiobadilika wa Iran.

Amesisitiza kuwa: “Hatutasitisha urutubishaji wetu. Hatuwezi na hatutakubali kukataa haki hii."

Ijumaa, wajumbe kutoka Iran na nchi tatu za Ulaya , Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani ,walikutana kwa raundi ya pili ya mazungumzo ya nyuklia katika ubalozi mdogo wa Iran jijini Istanbul, Uturuki.

Magari yaliyowabeba wajumbe hao yalionekana yakiingia katika majengo ya ubalozi. Mazungumzo hayo yanafanyika kwa faragha, bila kuwahusisha waandishi wa habari.

Iran inawakilishwa katika mazungumzo haya na Naibu Mawaziri wa Mambo ya Nje Majid Takht-Ravanchi na Kazem Gharibabadi.

Iran ilikubali kurejea kwenye meza ya mazungumzo hayo kufuatia ombi la nchi tatu za Ulaya ambazo ni wanachama wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 (JCPOA).