Satelaiti ya Iran, Nahid-2, yarushwa katika anga za mbali kwa mafanikio
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128748-satelaiti_ya_iran_nahid_2_yarushwa_katika_anga_za_mbali_kwa_mafanikio
Satelaiti ya mawasiliano na utafiti wa anga ya Iran, Nahid-2, iliyotengenezwa kikamilifu ndani ya nchi, imerushwa kwa mafanikio kuelekea anga za mbali Ijumaa, Julai 25, kwa kutumia roketi ya Kirusi ya Soyuz.
(last modified 2025-07-25T10:57:15+00:00 )
Jul 25, 2025 10:57 UTC

Satelaiti ya mawasiliano na utafiti wa anga ya Iran, Nahid-2, iliyotengenezwa kikamilifu ndani ya nchi, imerushwa kwa mafanikio kuelekea anga za mbali Ijumaa, Julai 25, kwa kutumia roketi ya Kirusi ya Soyuz.

Operesheni ya kuirusha imefanyika katika Kituo cha Vostochny Cosmodrome nchini Russia, ikiwa ni sehemu ya misheni ya pamoja iliyojumuisha setilaiti za Ionosfera-M3 na M4 za Russia, pamoja na satelaiti nyingine 18 kutoka mataifa mbalimbali.

Kilichoonekana kama hatua muhimu kwenye operesehni hiyo ni kuwepo kwa nembo ya Shirika la Anga la Iran (ISA) kwenye roketi ya Soyuz — ishara ya ushiriki rasmi wa Iran katika misheni ya kimataifa ya anga za mbali.

Roketi ya Soyuz imewahi kubeba satelaiti kadhaa za Iran hapo awali, zikiwemo Khayyam, Pars-1, na Hodhod.

Nahid-2 imeundwa kukaa kwenye obiti kwa kipindi cha miaka mitano. Changamoto kuu kwa satelaiti zinazodumu muda mrefu angani ni kudidimia kwa obiti kwa sababu ya mvutano wa sayari ya dunia, hali inayoweza kuathiri nafasi na utendaji wa setilaiti. Ili kukabiliana na hilo, Nahid-2 imefungwa mfumo wa msukumo uliobuniwa na kutengenezwa nchini Iran, unaoweza kurekebisha urefu wa obiti kwa hadi kilomita 50.

Wahandisi wa anga za mbali wa Iran walibuni na kutengeneza mfumo huo wa msukumo kikamilifu hapa nchini. Setilaiti hiyo hutumia injini ndogo za msukumo wa gesi moto zilizotengenezwa nchini, zikiwa na vipengele vya hali ya juu kama vile tanki la mafuta la mchanganyiko (composite), vali za shinikizo la juu, na mfumo wa usahihi wa udhibiti wa mwelekeo.

Vipuri hivi ni vya teknolojia ya hali ya juu na kwa kawaida havipatikani kirahisi kwenye masoko ya kimataifa jambo linaloonesha uwezo wa ndani wa Iran katika sekta ya teknolojia ya juu.

Mbali na mfumo wa msukumo, Nahid-2 pia inafaidika na teknolojia zingine za kiufundi zilizotengenezwa ndani ya nchi. Hii ni pamoja na mipako maalum ya polima na gundi za kiwango cha anga za mbali, ambazo husaidia kudhibiti joto na usambazaji wa umeme ndani ya injini na kwenye mwili wa setilaiti. Vifaa hivi vyote vilitengenezwa na taasisi za utafiti ndani ya Iran.

Aidha, setilaiti hiyo ina betri za lithiamu-ion zilizotengenezwa nchini Iran, ambazo zimeundwa kuhimili maelfu ya mizunguko ya kuchaji na kutoa chaji katika kipindi chote cha maisha ya setilaiti hiyo.