Refa bora wa Kisomali aliyezuiwa kuingia Marekani alakiwa kishujaa nyumbani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139032-refa_bora_wa_kisomali_aliyezuiwa_kuingia_marekani_alakiwa_kishujaa_nyumbani
Omar Abdulkadir Artan mwamuzi mashuhuri wa kandanda kutoka Somalia amelakiwa kishujaa wakati alipowasili nchini humo hii leo baada ya kuzuiwa kuingia Marekani; uamuzi ambao umemzuia kuchezesha katika mashindano ya Kombe la Dunia la Kandanda la FIFA mwaka huu.
(last modified 2026-06-10T10:46:31+00:00 )
Jun 10, 2026 10:43 UTC
  • Omar Artan FIFA wa Somalia akilakiwa kishujaa nchini humo baada ya kuzuiwa na Marekani
    Omar Artan FIFA wa Somalia akilakiwa kishujaa nchini humo baada ya kuzuiwa na Marekani

Omar Abdulkadir Artan mwamuzi mashuhuri wa kandanda kutoka Somalia amelakiwa kishujaa wakati alipowasili nchini humo hii leo baada ya kuzuiwa kuingia Marekani; uamuzi ambao umemzuia kuchezesha katika mashindano ya Kombe la Dunia la Kandanda la FIFA mwaka huu.

Omar Artan  anasifika sana kuwa miongoni mwa marefa bora zaidi barani Afrika.

Omar Abdulkadir Artan, mwenye umri wa miaka 34, alizuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami nchini Marekani na kurejeshwa alikotoka.

Inaripotiwa kuwa alisafiri kutoka Kenya, akapitia Uturuki, na kutua Miami, lakini mara tu alipowasili alizuiwa kuingia na kurejeshwa bila kuelezwa sababu.

Maafisa wakuu wa serikali, akiwemo Waziri wa Michezo wa Somalia Mohamed Abdulkadir Ali, Waziri wa Ulinzi Ahmed Moalim Fiqi, na maafisa wakuu kutoka Shirikisho la Soka la Somalia leo walimkaribisha mwamuzi Omar Artan katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Adan Adde katika mji mkuu Mogadishu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili Mogadishu, Artan alisema kuwa na hapa ninamnukuu: "Ninaweza kuwaahidi kwamba nitachezesha Kombe la Dunia lijalo la FIFA, na ninaishukuru FIFA na wananchi wa Somalia kwa msaada wao.

Artan angekuwa mwamuzi wa kwanza wa Somalia kuwahi kuchezesha katika mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA.

"Licha ya yaliyojitokeza kwangu, lakini niko katika hali nzuri, na ninazingatia changamoto zinazofuata katika taaluma yangu ya kazi ya waamuzi wa kandanda," amesema mwamuzi mashuhuri wa kandanda wa nchini Somalia alipozungumza mbele ya waandishi wa habari baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Adan Adde katika mji mkuu Mogadishu.