Pezeshkian: Iran haitalegeza kamba, itasimama kidete kulinda taifa dhidi ya vitisho
-
Rais Masoud Pezeshkian
Rais Masoud Pezeshkian ametilia mkazo msimamo thabiti wa Iran dhidi ya tishio lolote, akisema Jamhuri ya Kiislamu haitarudi nyuma wala kusita kulinda usalama na amani ya taifa lake.
Katika ujumbe uliotumwa kwenye akaunti yake rasmi ya X siku ya Jumatatu, Pezeshkian alisema kipaumbele kikuu cha Iran bado ni kulinda usalama wa taifa na kuhakikisha utulivu wa taifa la Iran.
"Tutatetea haki za taifa kwa nguvu zote na hatutarudi nyuma kutokana na tishio lolote."
Amesema "diplomasia na ulinzi" vinaunda vipengele viwili muhimu vya nguvu ya taifa, akieleza kuwa Iran haijaacha uwanja wa vita wala meza ya mazungumzo.
Rais Pezeshkian ameeleza imani yake kwamba kupitia umoja wa kitaifa na busara, Iran itafanikiwa kuondoka katika changamoto zilizopo sasa.
Ujumbe wa Rais Pezeshkian unafuatia mfululizo wa mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) siku ya Jumapili yakilenga maeneo yanayokaliwa kwa mabavu huko kaskazini kwa Israel.
IRGC imesema operesheni hiyo ni jibu kwa "uhalifu mkubwa" wa Israel kusini mwa Lebanon, ikiwa ni pamoja na mauaji na kuwalazimisha raia kuhama makazi yao, na kwamba kambi ya jeshi la anga ya Israel ilizopigwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzii ya Kislamu ilikuwa ikitumiwa kwa ajili ya uchokozi dhidi ya Lebanon.
Jana Jumatatu pia, IRGC ilishambulia kambi za kimkakati za Israel za Nevatim na Tel Nof katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel) baada ya mashambulizi ya Israel dhidi ya miji kadhaa ya Iran.
Maafisa wa Iran wamesisitiza mara kwa mara kwamba usitishaji mapigano kati ya Iran na Marekani, ulioanza kutekelezwa Aprili 8, ulikuwa na masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano katika pande zote, ikiwemo Lebanon.
Hata hivyo maafisa wa Iran wanasema, Israel, kwa ruhusa ya Marekani na kimya cha mashirika ya kimataifa, imeendeleza "vitendo vyake vya uovu" dhidi ya watu wa Lebanon kila siku, ikifanya uhalifu wa kivita kwa kutumia silaha zilizopigwa marufuku, ikiwa ni pamoja na mabomu ya fosforasi.