Congo DR : M23 yatishia kususia mchakato wa amani kama wafungwa hawataachiliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128798-congo_dr_m23_yatishia_kususia_mchakato_wa_amani_kama_wafungwa_hawataachiliwa
Kundi la waasi wa M23, ambalo linadhibiti maeneo mengi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, limetishia kususia mchakato wa amani unaoendelea sasa kutokana na suala la kuachiliwa kwa wafungwa jambo ambalo Kinshasa inachelewa kufanya.
(last modified 2025-07-26T23:04:57+00:00 )
Jul 26, 2025 23:04 UTC
  • Congo DR : M23 yatishia kususia mchakato wa amani kama wafungwa hawataachiliwa

Kundi la waasi wa M23, ambalo linadhibiti maeneo mengi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, limetishia kususia mchakato wa amani unaoendelea sasa kutokana na suala la kuachiliwa kwa wafungwa jambo ambalo Kinshasa inachelewa kufanya.

Huku mazungumzo ya amani yakitarajiwa kuanza tena mjini Doha, Qatar, mwezi ujao, Katibu Mkuu wa M23, Benjamin Mbonimpa, amesema: "Baada ya utekelezaji wa Azimio la Kanuni, majadiliano yatafuata mara moja ili kusaini makubaliano halisi.”

Azimio hilo, lililotiwa saini na pande zote mbili mapema mwezi huu, linatazamwa kama ramani ya njia ya kuelekea kwenye makubaliano ya amani ya kudumu ambayo yanatarajiwa kufikiwa tarehe 18 Agosti.

"Tutafanya nini huko Doha ikiwa wafungwa wetu bado hawajaachiliwa, kwa sababu imeandikwa katika Azimio kwamba kifungu hiki lazima kitekelezwe kabla ya kuendelea na hatua inayofuata," amesema Mbonimpa.

Makubaliano hayo yaliyotiwa saini mjini Doha chini ya upatanishi wa Qatar, yalipendekeza usitishaji mapigano mara moja.

Hata hivyo usitishaji huo wa mapigano ulikuwa ya muda mfupi huku pande zinazozozana zikilaumiana kwa ukiukaji wake.

Mapigano kati ya M23 na makundi ya kujilinda yanayojulikana kama Wazalendo, yanayoshirikiana na jeshi la serikali ya Congo, yanazidi kushika kasi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini.