UN yasema kunyimwa dhamana Besigye na mahakama ya Uganda kunatia hofu kubwa
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, (OHCHR), imesema mwenendo wa Mahakama Kuu ya Uganda wa kumnyima dhamana mara kwa mara kiongozi mkongwe wa upinzani nchini humo Kizza Besigye pamoja na msaidizi wake Obeid Lutale katika kesi inayowakabili ni jambo linalotia hofu kubwa.
Kupitia msemaji wake Liz Throssell, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imeeleza kwamba, mnamo tarehe 8 ya mwezi huu wa Agosti Besigye na Lutale walinyimwa dhamana kwa mara ya tatu, tangu watekwe nyara nchi jirani ya Kenya na kurejeshwa kinguvu nchini Uganda mwezi Novemba mwaka jana.
Akizungumza mjini Geneva, Bi. Throssell amebainisha kuwa, katika kukataa ombi lao la hivi karibuni la dhamana, Mahakama Kuu ya Uganda imedai kuwa hawastahili kupewa dhamana ya lazima kwa misingi kwamba wako rumande katika gereza la kiraia kwa muda usiozidi siku 180 zinazohitajika ili kustahili kuachiliwa kwa dhamana ya lazima.
Msemaji wa OHCHR ameongeza kuwa, mahakama haikuzingatia kunyimwa kwao uhuru kabla ya hapo kufuatia kutekwa nyara nchini Kenya na kurejeshwa kwa nguvu huko Uganda.
Kwa muktadha huo amesema: "tunazitaka mamlaka zitafakari upya uamuzi huo na kuwapatia dhamana, na kuhakikisha kuwa mashtaka yoyote dhidi yao yanafuata kikamilifu sheria za kimataifa za haki za binadamu".
Besigye na msaidizi wake walikamatwa tarehe 16 Novemba mwaka 2024 nchini Kenya na kurejeshwa kinguvu huko Uganda na baadaye kuzuiliwa bila kuwepo taarifa zake zozote kabla ya kufikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi mjini Kampala, tarehe 20 Novemba ambako alishtakiwa kwa makosa ya umiliki wa silaha na kuhatarisha usalama, yanayoweza kupelekea ahukumiwe adhabu ya kifo…/