Human Rights Watch yakosoa kitendo cha Burkina Faso kumfukuza afisa wa UN
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa uamuzi wa serikali ya kijeshi ya Burkina Faso kumfukuza mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Carol Flore-Smereczniak, na kumtangaza kuwa "mtu asiyetakikana," nchini humo na kutoa wito kwa mamlaka ya kijeshi kushirikiana na Umoja wa Mataifa badala ya "kuficha ukiukwaji wa haki za binadamu."
Uamuzi wa kumfukuza mwakilishi mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burkina Faso umechukuliwa baada ya kutolewa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu ukiukaji wa haki za watoto nchini humo.
Flore-Smereczniak ni afisa wa pili wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kufukuzwa na baraza la kijeshi la Burkina Faso, baada ya kutimuliwa Barbara Manzi mnamo 2022, suala ambalo Human Rights Watch inasema "linaangazia kuongezeka mwenendo wa serikali wa kutostahamili uangalizi huru."
Msemaji wa baraza la kijeshi la Burkina Faso amemshutumu mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa kushiriki katika utayarishaji wa ripoti ya mwezi Aprili, ambayo ilisajili athari mbaya za vita kwa watoto nchini Burkina Faso.
Utawala wa kijeshi wa Burkina Faso umepinga matokeo ya ripoti hiyo, ambayo yameilaumu serikali, wanamgambo wanaoliunga mkono jeshi, na makundi ya waasi yenye silaha kuwa yanahusika na ukiukaji wa haki za binadamu.
Ripoti hiyo imesajili "ukiukaji mkubwa" 2,483 dhidi ya watoto 2,255, ikiwa ni pamoja na mauaji, utekaji nyara na kuajiri au kutumiwa watoto na vikundi vyenye silaha na vikosi vya usalama, kati ya Julai 2002 na Juni 2024.
Ripoti hiyo pia imebainisha ongezeko la mashambulizi dhidi ya shule na kueleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuzuiliwa watoto kwa madai ya kuwa na uhusiano na makundi yenye silaha.