Amnesty International: Haki za binadamu zimekiukwa mashariki mwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129826-amnesty_international_haki_za_binadamu_zimekiukwa_mashariki_mwa_kongo
Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, limezituhumu pande zinazozozana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kufanya ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na vitendo vya kubaka kwa umati, mauaji ya kiholela na utekaji nyara.
(last modified 2025-10-16T03:06:03+00:00 )
Aug 22, 2025 02:12 UTC
  • Amnesty International: Haki za binadamu zimekiukwa mashariki mwa Kongo

Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, limezituhumu pande zinazozozana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kufanya ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na vitendo vya kubaka kwa umati, mauaji ya kiholela na utekaji nyara.

Katika uchunguzi wake wa karibuni, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeripoti kuwa waasi wa M23 na kundi la wanamgambo wenye mfungamano na serikali ya Kinshasa kwa jina la "Wazalendo" wamewabaka wanawake na kufanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia mashariki mwa Kongo. 

"Ukatili wa pande zinazopigana hauna mipaka. Ukatili huu unalenga kuwatesa, kuwatisha na kuwadhalilisha raia huku kila upande ukijaribu kuwa na udhibiti," amesema Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International katika eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika. 

Kundi la waasi la M23 linadhibiti eneo kubwa mashariki mwa Kongo, ikiwa ni pamoja na makao makuu ya majimbo yaani Goma na Bukavu.

Umoja wa Mataifa, serikali ya Kinshasa na pande nyingine kadhaa zinaituhumu nchi jirani ya Rwanda kuwa inawasaidia waasi wa M23, tuhuma ambazo zimekanushwa na Kigali.