Viwiliwili visivyopungua vitano vya wahanga wa itikadi kali za kidini vyafukuliwa Kenya
Viwiliwili visivyopungua vitano vimefukuliwa kutoka kwenye makaburi yenye kina kifupi katika eneo moja la pwani kaskazini ya Kenya, ambako wahanga wa itikadi kali za kidini wanashukiwa kuwa walizikwa.
Kamishna wa Kaunti ya Kilifi Josephat Biwott amevieleza vyombo vya habari kuwa viwiliwili vya watu hao watano vimepatikana katika makaburi manne na akaongeza kuwa wamepata miili zaidi katika maeneo mengine 27.
Afisa wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Robert Kiinge amesema, maafisa husika walikuwa wamechimba karibu maeneo 27 kwenye ukanda huo wa pwani katika eneo la ekari tano karibu na kijiji cha Binzaro, huko Kilifi na kwamba hadi sasa wamepata miili hiyo mitano.
Zoezi la kufukua miili hiyo lingali inaendelea katika eneo hilo lililoko viungani mwa mji wa Malindi, karibu na eneo la Shakahola ambako mamia ya waumini waliokuwa wanashurutishwa kufunga, walipatikana wakiwa wamefariki, miaka miwili iliyopita.
Itakumbukwa kuwa, mnamo mwezi Julai, afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ya Kenya ilisema inaamini wahanga waliozikwa katika eneo hilo, walilazimishwa kufunga kutokana na kushiriki na kuamini itikadi kali za kidini. Washukiwa 11 wanachunguzwa kuhusiana na vifo hivyo.
Zaidi ya watu 400 walikufa kwenye moja ya mikasa mibaya zaidi na ya kusikitisha zaidi nchini Kenya uliohusisha waumini wa itikadi kali za kidini uliotambulika kama "Mauaji ya Msitu wa Shakahola" na miili yao ilifukuliwa kwenye mji wa Malindi.
Kisa hicho kiligonga vichwa vya habari si nchini Kenya pekee bali pia ulimwenguni kote. Mchungaji Paul Mackenzie aliyekuwa kiongozi wa waumini hao, ambaye aliwahimiza kufunga hadi kufa ili waingie mbinguni, hivi sasa anakabiliwa na kesi huko mjini Mombasa, hata hivyo amekana kufanya kosa lolote la mauaji.../