Shambulizi la droni Sudan lateketeza malori 16 ya Umoja wa Mataifa
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, shambulizi la droni katika msafara umesababisha kuteketea kwa malori 16 ya misaada iliyokuwa inahitajika mno katika eneo la Darfur Kaskazini nchini Sudan, lililokumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Msemaji wa Umoja wa mataifa Daniela Gross amewaambia waandishi wa habari kuwa madereva wote na maafisa waliokuwa wanasafiri na Shirika la Chakula Duniani, WFP, wako salama.
Afisa huyo wa aUmoja wa Mataifa amesema haijawa wazi bado ni kundi lipi lililohusika na shambulizi hilo ambalo ni la pili katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ambalo limezuia msafara wa Umoja wa Mataifa kuwasilisha misaada huko Darfur Kaskazini.
Mapema mwezi Juni mwaka huu, msafara wa Shirika la Mpango waa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), ulishambuliwa wakati ulipokuwa unasubiri kuidhinishwa kuelekea makao makuu ya Darfur Kaskazini, el-Fasher, na watu watano wakafariki dunia na wengine kujeruhiwa.
Mgogoro kati ya jeshi la Sudan SAF na Vikosi vya Msaada wa Harakati RSF umepelekea kuzuka mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani na ambao unazidi kuwa mbaya siku baada ya siku kutokana na juhudi za upatanishi kutozaa matunda.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vilianza Aprili 2023 kutokana na mvutano wa kuwania madaraka kati ya makamanda wa jeshi na wa RSF. Mapigano hayo yameiharibu nchi hiyo ya Afrika, yamewalazimisha watu wapatao milioni 14 kuyahama makazi yao na kusababisha baadhi ya maeneo kukumbwa na baa la njaa.