Uganda yaafiki kuwapokea wahamiaji waliotimuliwa Marekani kama hawana rekodi za uhalifu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129886-uganda_yaafiki_kuwapokea_wahamiaji_waliotimuliwa_marekani_kama_hawana_rekodi_za_uhalifu
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda imesema, nchi hiyo itakubaliana na mpango wa Marekani wa kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa nchini humo ikiwa hawatakuwa na rekodi za uhalifu au si watoto wasio na jamaa zao.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
Aug 23, 2025 06:01 UTC
  • Uganda yaafiki kuwapokea wahamiaji waliotimuliwa Marekani kama hawana rekodi za uhalifu

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda imesema, nchi hiyo itakubaliana na mpango wa Marekani wa kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa nchini humo ikiwa hawatakuwa na rekodi za uhalifu au si watoto wasio na jamaa zao.

Wizara hiyo imeeleza hayo katika taarifa ambayo ilitoa siku ya Alkhamisi na kuongeza kwamba makubaliano hayo yamekamilika lakini masharti yake yanaendelea kuchunguzwa.

Taarifa hiyo imeendelea kubainisha kuwa Kampala inapendelea wahamiaji watakaopelekwa huko wawe wa mataifa ya Kiafrika, lakini haijafafanua zaidi kile ambacho nchi hiyo inaweza kupata kwa kukubali kuwapokea wahamiaji hao waliofukuzwa nchini Marekani.

Ubalozi wa Marekani nchini Uganda umekataa kutoa maelezo kuhusu kile ulichokiita "mazungumzo ya kidiplomasia," lakini umesema wanadiplomasia wanataka kuunga mkono sera ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kuwaweka Wamarekani salama.

Hata hivyo, baadaye huko mjini Washington, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alikuwa amezungumza kwa simu na Rais wa Uganda Yoweri Museveni kuhusu kadhia hiyo ya uhamiaji na masuala mengine kadhaa.

Serikali ya Trump inadai kuwa imekuwa ikitafuta njia za kuwazuia wahamiaji kuingia Marekani kinyume cha sheria na kuwafukuza wale ambao tayari wameshafanya hivyo, hasa wale walio na rekodi za uhalifu na wakiwemo wale ambao hawawezi kufukuzwa kirahisi na kurejeshwa nchini mwao.

Wanaharakati wa haki za binadamu wamekosoa makubaliano hayo ya Washington na Kampala ya kuwapokea raia wa kigeni wanaotimuliwa nchini Marekani na kusema yamkini ukawa unahalifu sheria za kimataifa.

Wakili wa kutetea haki za binadamu nchini Uganda Nicholas Opio ameufananisha mpango wa kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa huko Marekani na magendo ya binadamu na kueleza kwamba utaiweka mashakani hatima ya watu hao.../