UN: DRC inakabiliwa na moja ya hali mbaya zaidi za kibinadamu duniani
Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakabiliana na mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, huku machafuko na ukosefu wa usalama vikiendelea kuwaangamiza raia mashariki mwa nchi hiyo.
Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Martha Ama Akyaa Pobee, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa anayehusika na Afrika katika Idara za Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani na Operesheni za Amani, amesema: "Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa sasa inakabiliwa na moja ya hali mbaya zaidi za dharura za kibinadamu duniani. Uhaba wa chakula unaongezeka huku familia zikipoteza uwezo wa kufikia mashamba yao na kuona mavuno yao yakinyakuliwa".
Huku akiashiria kuongezeka kwa hali mbaya ya kubaki bila makazi, Pobee amesema: "leo hii, Wakongomani milioni 5.9 ni wakimbizi wa ndani, ikiwa ni pamoja na milioni moja Kivu Kaskazini na milioni 1.5 Kivu Kusini. Familia hutimuliwa mara kwa mara na kujikuta kila mara kwenye mzunguko wa hofu na hali ya kuhama".
Wakati hatua za kidiplomasia zilizopigwa hivi karibuni zimeleta matumaini, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwezi Juni na Julai kwa uwezeshaji wa Marekani na Qatar, Pobee ametahadharisha kwamba "mabadiliko ya hali ya usalama mashinani hayalingani na maendeleo yaliyofikiwa katika nyanja ya kidiplomasia."
Afisa huyo wa UN amesema: "idadi ya majeruhi wa kiraia imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Wafanyakazi wa huduma za kibinadamu wanahatarisha maisha yao ili kutoa usaidizi mdogo kwa idadi ya watu ambao mahitaji yao yanaendelea kuongezeka. Unyanyasaji wa kingono unaohusiana na mgogoro uliopo unaendelea huku kukiweopo na hali ya kila mtu kutojali. Na utumikishaji wa watoto kwa nguvu vitani ungali unaendelea".../